Makala

'Upanzi wa matikitimaji unahitaji uchimbaji makoongo makubwa'

August 7th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MATIKITIMAJI hufanya vyema katika maeneo yenye joto jingi.

Wataalamu wa kilimo wanasema hali hii ya hewa inafanya pia yawe na ladha tamu.

Kiwango cha joto – kipimo cha sentigredi – kinachopendekezwa ni kati ya nyuzi 22 na 28.

Kulingana na mtaalamu Peter Otieno kutoka kitengo cha Mimea, Kilimomseto na Udongo, Chuo Kikuu cha Egerton, matikitimaji yananawiri maeneo yaliyo mita 1500 juu ya ufuo wa bahari.

Mdau huyu anasema kiwango cha mvua kinachopendekezwa ni milimita 400-600 kwa mwaka.

Aidha, maeneo yasiyopokea mvua ya kutosha, mfumo wa unyunyiziaji maji mashamba kwa mifereji hususan kwa wenye bwawa, vidimbwi au kiini chochote kile cha maji, wanahimizwa kuyakuza.

“Maji yakizidi, husababisha ugonjwa wa majani na kulemaza shughuli za uchanaji maua,” anaeleza Bw Otieno.

Matunda haya yanakua vyema kwenye udongo usiotuamisha maji.

Kiwango chake cha asidi, pH, kinapaswa kuwa cha wastani, 6.0 au 6.5 kikiwa bora zaidi.

Maeneo yanayozalisha matunda haya kwa wingi nchini ni Machakos, Kajiado na Pwani mwa Kenya. Thika na Meru pia huyakuza, ingawa si kwa wingi.

Bw Zachariah Onchuru ‘Ken Kilifi’, ni mkuzaji wa matikitimaji eneo la Pwani. Katika shamba lake lenye ukubwa wa ekari 10 kijiji cha Chakama, Magarini, barobaro amelipamba kwa matunda na mboga asili kama vile mchicha na mnavu.

Bw Zachariah Onchuru ‘Ken Kilifi’, ni mkuzaji wa matikitimaji eneo la Pwani. Picha/ Sammy Waweru

Kuna njia mbili za kuyapanda kwa mujibu wa maelezo ya mkulima huyu; kupanda mbegu moja kwa moja shambani au kuzitunza kitaluni ili kupata miche, ambayo huhamishiwa eneo la upanzi.

“Njia bora na isiyo na kikwazo ni kupanda mbegu moja kwa moja,” anasema Bw Onchuru.

Mkulima huyu anatumia mfumo mpya maarufu kama ‘Masterpits’ katika kuzalisha matikitimaji. Ni mfumo wa kuchimba makoongo makubwa, yanayositiri mimea kadhaa na ambayo yameandaliwa kwa njia inayozuia uvukizi wa maji na mmomonyoko wa udongo.

Mbali na kutumika kukuza matunda haya, Onchuru anasema pia yanaweza kutumika katika upanzi wa maboga, egg plants, sukumawiki, matango na vitunguu.

Shamba linapolimwa na kuandaliwa sambamba, mashimo-masterpits yenye urefu wa sentimita 30 kuenda chini na upana wa sentimita 45 huandaliwa.

“Katika kila laini, yawe na nafasi ya mita mbili kutoka shimo moja hadi lingine na laini pia ziwe na nafasi ya mita mbili kati yake,” anafafanua mkulima huyu.

Mbolea, ya mifugo huwekwa mle na kuchanganywa vyema na udongo uliotolewa shimoni.

Bw Onchuru anasema ekari moja inasitiri mashimo 1,200 kila shimo likipandwa punje nne za mbegu. Zinapandwa kwenye vijishimo vidogo, shomoni, vikipendekezwa kuwa sentimita 3-4.

Maji ni kiungo muhimu katika kilimo cha matikitimaji na Bw Otieno anashauri yanyunyiziwe kwa kipimo.

“Maji mengi huharibu ladha ya matikitimaji, pamoja na kusababisha yaoze,” Otieno anaonya.

Mbali na maji, mitikitimaji yatunzwe kwa mbolea na fatalaiza.

Kando na kudhibiti uvukizi wa maji na mmomonyoko wa udongo, Onchuru anasema mfumo wa Masterpits pia unapunguza gharama, kuongeza mazao ikiwa ni pamoja na kuepushia mkulima kizungumkuti cha mzunguko wa mimea.

“Mkulima anaweza kuza matikitimaji katika eneo moja kwa zaidi ya misimu kumi. Anachopaswa kufanya ni kubadilisha anakochimba mashimo,” aeleza Bw Onchuru. Matunda haya huanza kuzalisha kati ya siku 65 hadi 90.

Kupitia matunzo bora kitaalamu, mtikitimaji mmoja unaweza kuzalisha matunda mawili, yenye wastani wa kilo nane kila moja.

Magonjwa yanayoathiri matunda ndiyo hushuhudiwa katika kilimo cha matikitimaji. Wadudu pia huyadunga, suala linaloyafanya kukataliwa sokoni na hata kusababisha yaoze.

Bw Onchuru anasema Machi 2019 matunda yake yalihangaishwa na magonjwa na kiangazi, ambapo alikadiria hasara isiyomithilika.

“Sijafa moyo,” anasema.

Wakulima wanahimizwa kuwekeza miradi yao kwenye bima ili majanga yakitokea na kusababisha hasara, itakuwa rahisi kufidiwa.

“Mafuriko, magonjwa na hata wadudu ni baadhi ya changamoto zinazokumba wakulima. Ni muhimu wawekeze kilimo chao kwenye bima,” anashauri mtaalamu wa masuala ya fedha na uchumi, Bw Michael Muriuki.