Makala

Upanzi wa viazi kitaalamu

August 21st, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

VIAZI mbatata ni zao la pili lenye walaji wengi nchini na katika Ukanda wa Afrika Mashariki, likitanguliwa na mahindi.

Aidha, viazi hivi vinakadiriwa kuwa na zaidi ya wakulima 800,000 wanaovikuza katika mashamba madogo.

Vinatumika katika mapishi ya vibanzi almaarufu chipsi, na kripsi ambazo ni vipande vyembamba vya viazi vilivyochomwa kwa mafuta na kukaushwa.

Pia, viazi hivi huandaa vitoweo mbalimbali kama vile kwa kuvipika pamoja na nyama, kabichi na kwa maharagwe.

Chakula asili aina ya mukimo – mchanganyiko wa kande, majani ya maboga – huandaliwa kwa kuongeza viazimbatata, kisha ukapondwapondwa.

Ukuzaji, vinaaminika kustawi maeneo yanayopokea kiwango cha mvua milimita 900-1400 kwa mwaka. Kiwango cha joto kinakadiriwa kuwa kati ya nyuzi 10-23 sentigredi.

Aidha, wataalamu wa masuala ya kilimo wanapendekeza udongo uwe na asidi, pH 4.8 hadi 5.8.

Udongo, usituamishe maji. Huzalishia ardhini, maji yakizidi viazi vitakuwa katika hatari ya kuoza upesi.

Ni mimea inayosemekana kuweza kustahimili maeneo yenye baridi kali. Kenya, kaunti zinafahamika kuzalisha kwa wingi ni; Nyandarua, Meru, Nyeri, Kiambu, Taita Taveta, Nakuru, Narok na Bomet.

Pia, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia, Bungoma, Uasin Gishu na West Pokot, zinaorodheshwa miongoni mwa orodha ya kaunti hizo..

Nyandarua, ndiyo inaongoza nchini katika uzalishaji wa viazi hivi.

Kwa zaidi ya miaka mitano, Timothy Mburu amekuwa mkuzaji wa viazimbatata eneo la Naromoru, Kieni, Kaunti ya Nyeri.

Amepata tajiriba kukuza zao hili, kiasi cha kuibuka na mfumo wa kuzalisha mbegu bora.

Mkulima huyu hutumia mfumo wa unyunyiziaji maji mashamba kwa mifereji, ambapo ana bwawa linalofanikisha shughuli hiyo.

Bw Mburu huzalisha viazi hivi kwenye ekari nne, na anasema hufanya awamu sita kwa mwaka.

Shamba hulimwa kwa trekta. Upanzi wake ni wa mitaro, yenye urefu wa futi mbili kuenda chini nafasi ya mmoja hadi mwingine akiipa sentimita 75.

Upanzi, nafasi ya kiazi kimoja hadi kingine huipa kimo cha sentimita 30.

Bw Mburu hutumia mbolea-kinyesi cha mifugo kilichochanganywa na majani na matawi, kisha kikapewa muda wa miezi kadhaa ili kuiva sambamba, anamwaga juu ya mbegu alizopanda.

Anaeleza kwamba yeye ndiye hujitengenezea mbolea hiyo, maarufu kama mboji au vunde.

“Baada ya kupanda mbegu za viazi, huimwagilia juu yake. Mimea inayozaa viazi huchipuka ikielekea juu, hivyo basi kutia mbolea juu ya mbegu huistawisha na kuipa ari,” anafafanua.

Wiki mbili au tatu baada ya mbegu kuchipuka, mkulima huyu hufanya palizi ya kwanza.

Viazi huhitaji madini ya Nitrojini kwa wingi.

Pia, vinahitaji Potassium na Calcium.

Mtaalamu Lawrence Ngugi kutoka Hygrotech-kampuni inayozalisha mbegu za viazi na mboga, anahimiza wakulima kupanda viazimbatata kwa mbolea tele. “Mbolea ya mifugo imesheheni Nitrojini. Pia, ni muhimu miviazi itiwe fatalaiza yenye Potassium na Calcium ili kunawirisha mazao,” ashauri Bw Ngugi.

Naromoru ni eneo kame, linalopokea mvua kwa uhaba na Bw Mburu anasema hali hiyo si kikwazo katika kilimo cha viazi iwapo mkulima ana chanzo cha maji. “Maeneo kame ni vigumu viazi kuathiriwa na early na late bligh-magonjwa sugu kwa viazi. Hivyo basi huwa sipulizii dawa,” aeleza mkulima huyu ambaye pia ni mtaalamu.

Bw Mburu ana Stashahada ya Masuala ya Mazingira na Kilimomseto.

Mbali na magonjwa hayo ya baridi, msimu wa mvua viazi pia hutatizwa na bacterial wilt na magonjwa yanayohusishwa na udongo maji yanapozidi.

Viwavi, katika siku za kwanza kwenye ukuaji wa viazi na vithiripi, viazi vinapokomaa, ndio wadudu wanaoshuhudiwa mara kwa mara.

Kabla ya uchanaji maua, Bw Mburu hurejeshea miviazi udongo, hatua inayojulikana kama earthing up. “Hili hutia mimea motisha ili kutoa mazao mengi na makubwa,” asema.

Mkulima akizingatia taratibu zifaazo kitaalamu, siku 75 baada ya upanzi, viazi huwa tayari kuvunwa.

Ekari moja inahitaji magunia manane ya mbegu; moja likiwa na uzito wa kilo 110.

Mburu anasema ekari moja ina uwezo kuzalisha zaidi ya magunia 80.

“Kupata magunia 80 katika ekari moja ni jambo linalowezekana. Kila mmea kwa mujibu wa miaka ambayo nimekuza viazi nimegundua ukitunzwa vyema unaweza kuzalisha zaidi ya viazi 10,” akasema Bw Mburu.

Hata hivyo, Bw Meshack Wachira, mtaalamu kutoka Novixa International Ltd, anasema kinachofanya wakulima kutopata mazao ya kuridhisha ni kwa sababu ya kutofuata kanuni zifaazo katika shughuli za kilimo.

Mdau huyu anasisitizia haja ya mkulima kupimiwa udongo kabla ya kuanza kupanda viazi.

“Asidi, pH, kwenye udongo ni kigezo cha muhimu kutilia maanani katika kilimo cha viazi. Udongo usioafikia hitaji hilo, mkulima atashauriwa namna ya kuutibu,” asema Wachira.

Wateja wa Timothy Mburu huendea mazao shambani, maarufu kama ‘gate price’.

Kulingana na naye, hatua hii imemuwezesha kukwepa kero la mawakala, ambao hupakia kupita kiasi pamoja na kukandamiza bei.

“Bei ya lango, mkulima huweza kunadi mazao yake na kupata soko bora,” akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.

Suala la mawakala kuripotiwa kuhangaisha wakulima wa viazi Kenya si jambo geni.

Hata hivyo, kwenye mswada wa mazao, 2019, uliopitishwa na bunge la kitaifa Mei 2, changamoto zinazozingira wakulima wa viazi huenda zikadhibitiwa.