Jamvi La Siasa

Upatanishaji wa Uhuru, Gachagua washika kasi

February 25th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

JUHUDI za kuwaunganisha tena Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Rigathi Gachagua zimeshika kasi, hilo likitajwa kuwa sababu kuu ya viongozi hao kuanza kubadili misimamo yao mikali ya kisiasa waliyokuwa nayo hapo awali.

Jamvi la Siasa limebaini kuwa juhudi hizo zimekuwa zikiendeshwa na wazee na washirika wa karibu wa kisiasa wa viongozi hao wawili.
Juhudi hizo zimetajwa kuchangia Bw Gachagua kubadilisha msimamo mkali wa awali aliokuwa na dhidi ya Bw Kenyatta, ambapo sasa anashinikiza maelewano baina yao.

Kwenye mazishi ya Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw King’ori Mwangi katika eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri, Jumamosi iliyopita, Bw Gachagua alisema alikuwa akitamani kukutana na Bw Kenyatta ili “kusuluhisha tofauti zao”.

“Nimefika nikiwa nimechelewa kidogo kwa sababu nilikuwa nikihudhuria mazishi mengine katika Kaunti ya Kirinyaga. Nimeambiwa kuwa Bw Kenyatta alikuwa hapa. Yalikuwa matamanio yangu tukutane naye ili tusalimiane na kuondoa matatizo yoyote yaliyopo. Tofauti zilizozuka zilitokana na uchaguzi, ambao ushapita. Tunataka kuanza safari mpya ya umoja kwa watu wetu wa Mlima Kenya,” akasema Bw Gachagua.

Ijapokuwa Bw Kenyatta hakuzungumzia siasa kwenye hotuba yake kwa wazungumzaji, alisisitiza kuhusu umoja wa ukanda huo.

Pia, aliwaahidi washirika wa Bw Gachagua kwamba “atawaitia mbuzi” ili kuwa na kikao cha pamoja.

Ombi hilo lilitolewa na Gavana Mutahi Kahiga wa Kaunti ya Nyeri, ambaye ni mshirika wa karibu sana wa Bw Gachagua.

“Rais Mstaafu (Kenyatta), kile tunaomba ni utuite kwenye kikao ili tule mbuzi pamoja kama wazee….” akasema Bw Kahiga alipomsindikiza Bw Kenyatta kwenye gari lake.

“Sina shida. Nitawaita kwenye kikao hicho,” akasema Bw Kenyatta.

Bw Gachagua pia alitoa kauli kama hiyo, kwenye hotuba yake kwa waombolezaji.

“Rais Mstaafu (Kenyatta) ni kiongozi wetu. Ni kiongozi tunayemheshimu. Ni mtu aliyejiweza kifedha. Hatuwezi kujali akituita na kutuchinjia mbuzi ili kuzungumza kwa sauti moja kama wazee, eneo na jamii,” akasema Bw Gachagua.

Kutokana na hayo, duru zimeliambia Jamvi la Siasa kuwa kauli hizo zinatokana na juhudi za kichinichini za upatanishi ambazo zimekuwa zikiendeshwa na wazee, viongozi wa kidini, mabwanyenye na washirika wa kisiasa wa viongozi hao wawili.

Ripoti zilieleza kuwa ujumbe mkuu ambao washirika hao wamekuwa wakisisitiza ni kuhusu umuhimu wa umoja wa kisiasa wa Mlima Kenya, hasa uchaguzi mkuu 2027 unapokaribia.

“Ujumbe mkuu kwenye mazungumzo hayo ni hatari ya kisiasa inayolikabili eneo hilo kugawanyika. Ni hali ambayo ilishuhudiwa wakati wa utawala wa Rais Mstaafu (marehemu) Daniel Moi, ambapo jamii za Mlima Kenya zilikuwa kwenye upinzani kwa miaka 24. Hilo ndilo kosa tunalolenga kuepuka,” akasema mmoja wa wazee wanaoongoza juhudi hizo.

Sababu nyingine ambayo imetajwa kusukuma juhudi hizo ni midahalo ya kisiasa ambayo imeanza kujitokeza katika ukanda huo kuhusu ni nani anayefaa kuwa mgombea-mwenza wa Rais William Ruto ifikapo 2027.

Wale wanaoshiriki kwenye juhudi hizo wanasema kuwa wanahofia kuna “mkono wa nje” unaolenga kupanua migawanyiko iliyopo, baada ya baadhi ya viongozi kumpendekeza mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) kuwa mgombea-mwenza wa Dkt Ruto kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba ikiwa juhudi hizo zitafaulu, basi hayo yatakuwa manufaa makubwa kisiasa wa ukanda huo, kwani utakuwa umeimarisha na kuboresha usemi wake kisiasa.

Hata hivyo, wanaonya kuwa bado kitakuwa kibarua kigumu kuwapatanisha Bw Kenyatta na Bw Gachagua kutokana na tofauti zilizozuka baina yao kwenye uchaguzi wa 2022.