Habari za Kitaifa

Upepo mkali pwani ya Kenya kimbunga Hidaya kikitua Tanzania

May 4th, 2024 2 min read

ANTHONY KITIMO Na MARY WANGARI

SEHEMU mbalimbali katika fuo za Pwani ya Kenya zimeshuhudia upepo mkali na mawingu huku Tanzania ikiripoti kuathirika na kimbunga Hidaya.

Kikosi cha Walinzi wa Pwani Nchini kimekaa chonjo kwa athari za kimbunga hicho huku upepo mkali na mawimbi ya bahari yakiripotiwa katika Kaunti za Kwale na Kilifi.

Kikosi hicho kimeimarisha ulinzi katika maeneo yanayopakana na Bahari Hindi na kuweka mikakati ya kutoa usaidizi katika maeneo ya Kilifi, Mombasa, Shimoni, Lamu, Tana River na pia Garissa ambayo iko karibu na maeneo hayo ya mwambao wa Pwani.

Katika maeneo yaliyokaribu na bahari, kulionekana mawingu mazito wakati idara ya utabiri wa hali ya anga ikitangaza kuwa pwani itashuhudida kuongezeka kwa mawimbi yanayozidi mita 20 na upepo mkali.

“Tayari dalili za kimbunga zimeanza kushuhudiwa katika ukanda Pwani ya Kenya kwa kuongezeka kwa upepo mkali unaozidi kasi ya kawaida wa fundo 40 na mawimbi makubwa ya bahari juu ya mita 2 kwenda juu. Jitahadhari,” Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Kenya iliandika kwa mtandao wake.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alipiga marufuku shughuli zote za uvuvi, kuogelea na kubarizi katika fuo za pwani.

Waziri aliagiza kamati za usalama katika kaunti za pwani kushirikiana na Walinzi wa Pwani kutekeleza marufuku hiyo.

Katika nchi ya Tanzania, tayari mawimbi makali yameripotiwa siku moja tu bada ya kimbunga hicho kushuhudiwa nchini Comoros na hali hiyo inatarajiwa kuongezeka Jumapili asubuhi.

Hata hivyo, idara mbalimbali zinazopambana na majanga nchini zimetangaza kujitayarisha kwa tukio lolote ambalo linaweza kutokana na kimbunga hicho ambacho kinatarajiwa kabla ya Mei 6, 2024.

Mamlaka ya ubaharia nchini (KMA) ambayo iko na jukumu la kuratibu taasisi nyingine za kiserikali na zile zisizo za kiserikali, imesema imeweka mipango ya kuhakikisha uokoaji wa mali na binadamu unafanyika iwapo janga hilo litatokea.

“Hatutarajii kimbunga kikubwa huku Pwani ya Kenya ila ni mikakati tumeweka ili kupunguza makali yake iwapo kitatokea. Tumehakikisha shughuli za baharini kama uvuvi zimesitishwa hadi pale tutakapohakikishiwa bahari iko salama,” alisema Bw Julius Koech, mkurugenzi wa kitengo cha uokoaji na usalama KMA.

Bw Koech alisema KMA ikishirikiana na idara nyingine kama Kaunti ya Mombasa, serikali kuu, na shirika la Msalaba Mwekundu, imeweka maafisa katika sehemu mbali mbalimbali ili kutoa maagizo kwa wale wanaoishi katika fuo za pwani.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulidhihirisha kuwa maafisa wa polisi wametumwa katika fuo za pwani na sehemu za kuegeshea mashua za uvuvi ili kuhakikisha hakuna watu wanashiriki katika shughuli zozote baharini kwa sasa.

Siku ya Ijumaa, Rais William Ruto alitangaza kukaribia kwa tufani kali itakayopiga Pwani ya Afrika Mashariki na kuathiri hata bara.