Habari za Kaunti

Upepo mkali unavyochangia mabaharia wanaopotea nchi jirani kujipata Kenya


KUTOWEKATOWEKA kwa mabaharia, hasa wavuvi wa nchi ya Unguja wanapotelekeza shughuli zao baharini na kisha kupatikana Pwani ya Kenya, Lamu, limekuwa jambo la kawaida miaka ya hivi karibuni.

Kulingana na takwimu kutoka kwa Ubalozi Mdogo wa Unguja, kati ya visa viwili hadi vitano vya mabaharia wa nchi hiyo kupotea baharini na kisha kupatikana Kenya hurekodiwa karibu kila mwaka.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Dijitali, Balozi Mdogo wa Unguja, Bw Mohamed Farhan, anasema kila mara amekuwa akizuru Pwani ya Kenya ambapo amekuwa akishirikiana na vitengo vya kudhibiti usalama wa baharini kuwahoji, kuwapiga msasa, kuwapasisha na kisha kuwasafirisha wavuvi au mabaharia wake nchini kwao, Unguja.

Bw Farhan alisema wanaoripotiwa kutoweka nchini mwao hukaa baharini kwa karibu wiki tatu kabla ya ripoti za kupatikana kwao Pwani ya Kenya kujulikana.

Lakini je, kwa nini wavuvi na mabaharia wengine wa Unguja, Zanzibara na hata Tanzania huishia kupatikana Kenya punde wanapotoweka baharini nchini mwao?

Bw Farhan alifichua kuwa mara nyingi kutoweka kwa mabaharia hutokea wakati Bahari Hindi inaposhuhudia dhoruba inayochangiwa na upepo na mawimbi makali.

Balozi huyo alifafanua kuwa Kenya imekuwa kiokozi kikuu cha mabaharia hao kwa sababu punde upepo mkali unaposhuhudiwa baharini, mara nyingi huelekezwa maeneo ya Pwani ya Kenya ambapo makali yake hupungua.

Anasema wengi wa wale wanaotoweka wakiwa baharini nchini Unguja huwa ni wavuvi.

“Wakiwa baharini na mashua zao, ziwe ni kubwakubwa au ndogondogo, hujipata wakiandamwa na dhoruba na mawimbi makali. Upepo unaoshuhudiwa husukuma hivyo vyombo upande wa Pwani ya Kenya. Hata wakajaribu kupiga makasia kuvielekeza vyombo vyao mahali kwingine inashindikana. Upepo huvipeperusha kuvielekeza upande wa Pwani ya Kenya na kisha kutulia,” akasema Bw Farhan.

Aliongeza, “Cha kutia moyo ni kwamba hapa Kenya wanasaidiwa kwani huokolewa na usalama wao kudhibitiwa. Ni visa vichache ambapo utapata wavuvi wetu wakiwa wamefariki.”

Balozi huyo aliwashukuru walinda usalama na pia utawala wa Kenya kwa jumla kwa kile alichokitaja kuwa ni kuwaelewa na kuwatunza mabaharia wa nchi zingine wanaopotea na kisha kujipata Pwani ya Kenya.

“Hii Pwani ya Kenya, hasa Lamu ndilo eneo linalopokea sana sana wavuvi wetu wanaotoweka baharini. Ikumbukwe kuwa upepo wa Unguja hupiga au kuvuma kuelekezwa Pwani ya Kenya na hata kuelekea nchini Somalia,” akasema Bw Farhan.

Baadhi ya wazee wa Pwani waliohojiwa na Taifa Dijitali pia walitaja kuwepo kwa maeneo mengi ya Bahari Hindi iliyoko wazi nchini Unguja kuwa sababu tosha inayofanya vyombo vya baharini, iwe ni mashua, jahazi, au boti kukosa udhibiti wa kutosha, hivyo kuishia kusukumwa hadi Kenya.

“Ifahamike kuwa sehemu kama Lamu imejaa mikoko. Ni rahisi kwa mashua zinazosukumwa kutoka Unguja ambako kumesheheni bahari wazi na upepo mwingi kutia nanga Lamu kwani hapa kuna sehemu nyingi zilizojaa mikoko na miamba ya kuwawezesha wavuvi kutia nanga. Yaani Lamu ni kama ndiyo mwisho wa bahari ya upepo,” akasema Bw Omar Kassim, mkazi wa Kiunga.

Wiki iliyopita, wavuvi wawili kutoka Unguja walioripotiwa kutoweka baharini kwa siku 18 mwishowe waliokolewa katika eneo la Kui, karibu na Kiunga, Lamu Mashariki.

Wavuvi hao ni Farooq Abbas,26 na Ismael Ahmed,42.

Wawili hao wanatoka eneo la Mdomoni ndani ya kisiwa cha Anjoun, Unguja.

Agosti, 2021, watu saba raia wa Unguja walifariki huku wanane wakiokolewa mashua walimokuwa wakisafiria iliposombwa na dhoruba na mawimbi makali na kuharibiwa baharini.

Waliokolewa karibu na Watamu, eneo lililoko Pwani ya Kenya baada ya mashua yao kusukumwa na mawimbi makali kutoka Unguja.

Mei mwaka huu wakati nchi za Afrika Mashariki zikishuhudia athari za kimbunga Hidaya, mabaharia 22 kutoka Zanzibar waliokolewa kwenye Bahari Hindi Pwani ya Kenya mmoja akiripotiwa kufariki.

Mabaharia hao walikuwa wametoka wilaya ya Bagamoyo, Pwani ya Tanznania wakielekea Zanzibar kabla ya kukumbwa na upepo mkali baharini.

Baadhi ya mabaharia hao walipatikana Kwale, wengine Mombasa na kuna waliookolewa eneo la Kipini, kati ya Lamu na Tana River.