Habari Mseto

Upinzani mkali katika kongamano la uzazi

November 13th, 2019 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

KONGAMANO la Kimataifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo (ICPD), Jumanne liling’oa nanga licha ya kuwepo na upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kidini na mashirika ya umma.

Viongozi hao walihofia kuwa huenda lingetumiwa kujadili masuala yanayokiuka maadili na itikadi za Kiafrika.Kongamano hilo litakalokamilika kesho liliangazia afya ya uzazi, ustawi wa kijamii na uchumi na ukomeshaji wa visa vya ukeketaji wa wanawake.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza vita dhidi ya wanaume wanaowatia mimba watoto wa kike walio chini ya umri wa miaka 18.

Rais Kenyatta alisema serikali yake pia haitalegeza kamba katika vita dhidi ya ukeketaji wa wanawake na wasichana.

“Najitolea kuhakikisha kuwa tunamaliza visa vya ukeketaji na dhuluma nyinginezo dhidi ya wanawake. Tutakabiliana na mimba za mapema na kushirikiana na washikadau wengine kuwezesha wanawake kujistawisha kiuchumi,” akasema Rais Kenyatta.

Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa serikali ya Kenya, Denmark na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu (UNFA).

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni aliahidi kutenga fedha zaidi za kuwezesha wanawake na wasichana kupata huduma za kupanga uzazi.

Kongamano hilo lilipata pingamizi kutoka kwa viongozi wa kidini na mashirika ya umma, baada ya ratiba yake kuonyesha kuwa wahusika wangejadili kuhusu ushoga na usagaji.

“Makundi yaliyotengwa kama vile watu kutoka jamii ndogo, vijana, ambao hawajaoa, mashoga, wasagaji, watu wenye jinsia mbili na walemavu wangali wanapata changamoto ya kupata huduma za matibabu,” ikasema ratiba ya ICPD.Ratiba hiyo pia ingeangazia suala la kumaliza uavyaji mimba kwa njia zisizo salama.