Kimataifa

Upinzani wajiandaa kwa makabiliano na Magufuli

December 2nd, 2019 2 min read

NA GAZETI LA CITIZEN

VIONGOZI wa upinzani nchini Tanzania wameanzisha kampeni za kupigania uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kama njia ya kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao.

Chama hicho kinalenga kumpata mwaniaji maarufu atakayemtoa kijasho rais wa sasa John Magufuli.

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederic Sumaye, mwanasiasa mbishi na aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe ni kati ya wanasiasa maarufu ambao wanasaka nyadhifa za uongozi katika chama hicho kikubwa zaidi cha upinzani nchini Tanzania.

Wote hao, ambao ni wakosoaji wakubwa wa serikali ya Rais Magufuli, waliwasilisha karatasi zao za kuwania vyeo mbalimbali Ijumaa wiki jana.

Hata hivyo, ushindani mkali unatarajiwa kuwa kati ya Sumaye na Mbowe ambao watawania wadhifa wa uenyekiti.

Aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa alitumia chama hicho kugombea urais dhidi ya CCM ya Rais Magufuli mnamo 2015.

Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe pia anawania wadhifa huo ambao umekuwa ukishikiliwa na Mbowe tangu 2014 wakati chama hicho kiliandaa uchaguzi wake wa matawi mbalimbali na kiwango cha kitaifa.

Lowassa mapema mwaka huu alitangaza kwamba amerejea CCM na haijulikani iwapo atampinga Rais Magufuli kwenye uteuzi wa chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu mwakani.

Lissu, ambaye alikuwa nje ya taifa hilo akipokea matibabu kwa muda wa miaka miwili kutokana na jaribio la kumuua, atakuwa akiwania wadhifa wa naibu mwenyekiti dhidi ya mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea.

Akizungumzia uchaguzi huo, Mbowe alisema walimshawishi Lisu, ambaye wadadisi wanasema umaarufu wake unazidi kuongezeka, kuwania wadhifa wa naibu mwenyekiti.

“Binafsi sikuwa nataka kutetea wadhifa wangu wa uenyekiti lakini wafuasi na wajumbe wamenirai niwanie tena kutokana na jinsi ambayo nilikiongoza chama. Pia tulimshawishi Lisu awanie kwa sababu amejionyesha kama mwanasiasa anayepigania maslahi ya raia,” akasema Mbowe.

Kwa upande wake, Lisu alisema kwamba atashindana na Kubenea kuwania wadhifa wa Naibu Mwenyekiti na akapuuza kwamba wadhifa huo hauna umaarufu kama ule wa uenyekiti.

“Mimi nawania wadhifa ambao naona unanifaa kwa wakati huu. Sitahitaji kufanya kampeni dhidi ya mpinzani wangu kwa sababu nina imani wafuasi wa chama hiki watanipigia kura,” akasema Lisu.

Msomi na mshikilizi wa sasa wa wadhifa wa Naibu Mwenyekiti, Profesa Abdallah Safari ametangaza kwamba hatatea wadhifa wake ingawa akasisitiza kwamba atasalia kuwa mwanachama wa Chadema.

Viongozi hao wote kwa kauli moja wametoa wito kwa wafuasi wao kushiriki kampeni za amani na kukomesha uhasama dhidi ya wanachama wa zamani waliohamia CCM.