Michezo

Uprising yapaa hadi Ligi ya Taifa Daraja la Pili

July 15th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MBOTELA Kamaliza iliichapa Young Rovers bao 1-0 huku Uprising FC ikituzwa ushindi wa mezani na kumaliza kileleni mwa mechi za Kundi A kufukuzia taji la Nairobi East Regional League (NERL) msimu huu.

Uprising FC na Korogocho Youth washindi wa mechi za Kundi B zimetwaa tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu ujao.

Hata hivyo zimeratibiwa kukabiliana kwenye mchezo wa kutafuta bingwa wa kipute hicho msimu huu.

Uprising FC ambayo hunolewa na kocha, Collins Omondi ilinasa ushindi huo bila jasho baada ya wapinzani wao Tena United kusepa na kuingia gizani. Goli la Mbotela Kamaliza iliyopigiwa chapuo kubeba taji hilo lilifumwa kimiani na Vincent Chagala.

”Kusema kweli sina budi kushukuru wachezaji wangu kwa kujituma kiume kwenye mechi za mwisho walikofanya kweli na kuwapiku wapinzani wetu waliokuwa wamekuja kwa kasi,” kocha wa Uprising alisema.

Kwenye matokeo hayo, Nairobi Water iliigaragaza Dream Team magoli 4-0 kupitia Linus Okaro mabao mawili nao John Awalah na Humphrey Toboso waliifungia bao moja kila mmoja.

Nayo Creative Hands ilijikuta kwenye wakati mgumu iliponyukwa mabao 3-2 na FC Barca. Wafungaji wa FC Barca walikuwa Ezekiel Otieno, John Jontez’ Irungu na Derrick Omune. Kwenye jedwali, Uprising FC ilimaliza kileleni kwa alama 39, mbili mbele ya Mbotela Kamaliza.