Na STEPHEN ODUOR
UHABA mkubwa wa nyama ya ng’ombe umeanza kukumba vichinjio katika Kaunti ya Tana River, huku ukame ukizidi kuangamiza mifugo katika kaunti hiyo.
Kulingana na wauzaji nyama, ng’ombe waliokuwa wakichinjwa katika siku za hivi majuzi hawana afya bora na hivyo hawafai kwa biashara.Ng’ombe wengi wanaopatikana huwa wamekonda kutokana na ukosefu wa chakula na maji.
Bw Mohammed Salat, mmoja wa wafanyabiashara, alisema hakuna mwuzaji nyama anataka kuuza nyama ya ng’ombe.“Wengi wanaonelea heri wale nyama ya mbuzi. Mbuzi wananusurika na ukame kwa vile wanakula kila kitu ikiwa ni pamoja na majani ya vichaka vya miiba,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wamepandisha bei ya mbuzi maradufu ili kujaza gharama ya kutunza ng’ombe.Huku ng’ombe akiuzwa kwa Sh18,000 kutoka Sh40,000 mbuzi dume aliyekomaa aina ya Galla kwa sasa anauzwa Sh12,000 kutoka Sh7,500.
“Tunatumia Sh100 kununua lita 40 za maji kwa ng’ombe watatu. Ukiwa na ng’ombe 50, mbuzi 80 na kondoo wengine 40, inamaanisha unatakiwa kutumia zaidi ya Sh100,000 kila mwezi ili waweze kuishi,” akasema mfugaji Hassan Dumal.