Upungufu wa hela ulimsukuma Musalia kwa Ruto – Mbunge adai

Upungufu wa hela ulimsukuma Musalia kwa Ruto – Mbunge adai

NA BENSON AMADALA

MBUNGE wa Sabatia Alfred Agoi, amedai kuwa Kinara wa ANC Musalia Mudavadi, aliamua kufanya kazi pamoja na Naibu Rais Dkt William Ruto baada ya kukosa fedha za kufadhili kampeni zake za Urais.

Japo Bw Agoi alisema haukuwa uamuzi rahisi, ilimlazimu kinara wake ashirikiane na Dkt Ruto kwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta naye alikuwa ameamua kumuunga mkono Kinara wa ODM, Raila Odinga.

“Mwanzoni mikakati yetu ilikuwa kuhakikisha kuwa Musalia Mudavadi yupo debeni kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Hata hivyo, hakuwa na fedha za kutosha kuendesha kampeni kali,” akasema Bw Agoi.

“Tulimwambia kuwa wafuasi wake walikuwa wakimtaka aelekee debeni ila tatizo ni kuwa hatukuwa na fedha za kutosha kufanya kampeni ya kutisha kama ya Raila Odinga na Naibu Rais Dkt William Ruto. Njia pekee tuliyokuwa nayo ilikuwa kujiunga na kambi ya Dkt Ruto,” akaongeza.

Bw Mudavadi alitangaza kuwa chama chake kimejiunga na kambi ya Naibu Rais wakati wa Kongamano la Kitaifa Wajumbe (NDC) kule Bomas mnamo Januari 23.

Bw Agoi alikuwa akizungumza eneo la Kaskazini Mashariki mwa Bunyore kwenye eneobunge la Emuhaya mnamo Jumanne. Alisisitiza kuwa kilichomsukuma Bw Mudavadi kuingia kwenye kambi ya Dkt Ruto ni ukosefu wa fedha za kampeni.

Kenya Kwanza

Ufichuzi huo sasa unathibitisha kuwa huenda Naibu Rais ndiye atakuwa mgombeaji wa Urais wa Muungano wa Kenya Kwanza ingawa Bw Mudavadi na Kinara wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula, bado wanawataka wafuasi wao waamini kuwa, muungano huo bado haujamchagua mgombeaji wake wa Urais.

Baada ya kufarakana na kambi ya Bw Odinga chini ya muungano wa NASA, Bw Mudavadi na wandani wake walibuni muungano wa OKA pamoja na Kalonzo Musyoka wa Wiper na Gideon Moi wa Kanu.

Hata hivyo, ilipobainika kuwa angeingia kwenye ushirikiano na Dkt Ruto, Mabw Musyoka na Moi waliondoka kwenye NDC ya ANC, huku Bw Mudavadi naye akisema kuwa uamuzi wake ulitokana na nia ya kuwaokoa Wakenya kutoka uongozi mbaya.

Hatua yake hiyo, pamoja na baadhi ya wabunge wake kuham, kulipunguza zaidi umaarufu ambao ANC ilikuwa nao eneo la Magharibi. Wabunge hao walihamia chama kipya cha DAP-K huku ODM nayo pia ikiendelea kudhibiti siasa za Magharibi mwa nchi.

Wabunge waliohama ni Peter Nabulindo (Matungu), Christopher Aseka (Khwisero), Tindi Mwale (Butere), Titus Khamala (Lurambi) na Oku Kaunya (Teso Kaskazini).

Aidha, Bw Agoi alieleza kuwa njia pekee ya siasa za Bw Mudavadi kusalia hai, ilikuwa kujiunga na kambi ya Dkt Ruto ili wawe na nafasi kwenye serikali itakayoundwa.

Kauli yake sasa inakinzana na ile ya kiongozi wa chama chake ambaye amekuwa akisisitiza kuwa yupo debeni hata baada ya kuunda Kenya Kwanza.

You can share this post!

Kenya Kwanza wapiga abautani kuhusu mtaala

Matokeo ya KCPE kutolewa wiki 2 zijazo – Magoha

T L