Makala

Upungufu wa vifaranga nchini watishia wakulima

April 16th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

HUKU Sekta ya Kilimo ikikadiriwa kuchangia asilimia 25 ya ukuaji wa uchumi (GDP), ufugaji kuku unawakilisha asilimia 30 ya mchango huo.

Karibu kila boma, hususan wanaomiliki ploti, linaendeleza ufugaji kuku; uwe wa kukithi familia mayai na nyama, au, kuendeleza biashara.

Sekta ya ufugaji ikikadiriwa kuwa na mchango mkubwa, wakulima haswa wanaoshiriki biashara ya kuku na mayai, wanalalamikia uhaba wa vifaranga.

Wanapitia nyakati ngumu kupata vifaranga kutoka kwa wazalishaji.

Changamoto hii inaathiri kuku maalum wa nyama (broilers) na wale wa kienyeji walioboreshwa kutaga mayai na pia kwa minajili ya nyama.

Abisai Nandi, mwawasisi wa Chicken Basket Ltd, anasema gapu hiyo imeathiri biashara yake kwa kiwango kikubwa.

“Kwa muda wa miaka miwili mfululizo, kumekuwa na upungufu wa vifarfanga, unaothiriki kuku maalum wa nyama na wa kienyeji walioboreshwa kwa minajili ya mayai na nyama,” mfugaji huyo anasema.

Nandi Abisai, mwawasisi wa Chicken Basket Ltd, kampuni ya kufuga kuku Kisumu akiwalisha kwenye vizimba. PICHA|SAMMY WAWERU

Chicken Basket, ni kampuni ya ufugaji kuku wa kienyeji walioboreshwa, na Abisai hutoa huduma katika Kaunti ya Kisumu, Siaya, Kakamega, na Vihiga.

Aidha, ana mradi unaojulikana kama Choma Preneurship, anaotumia kupiga jeki vijana wanaochuuza bidhaa za kuku kama vile mayai, vipande vya nyama na soseji kwa kutumia troli.

Steve Sande, Afisa Mkuu Mtendaji Kamsa Poultry Ltd, kampuni ya ufugaji kuku Kisumu pia analalama kuhusu uhaba wa vifaranga.

“Biashara yangu imeathirika pakubwa kwa sababu ya upungufu wa vifaranga hasa wenye umri wa mwezi mmoja,” Sande anaarifu.

Mfugaji huyu anahimiza haja ya wadauhusika na serikali kwa jumla kuhakikisha wakulima wanapata vifaranga bora; kwa kuboresha miundomsingi.

Steve Sande, Afisa Mkuu Mtendaji Kamsa Poultry Ltd. PICHA|SAMMY WAWERU

Ufanisi katika ufugaji wa kuku unategemea uwepo wa vifaranga bora na waliochanjwa.

Upungufu wa makinda ya kuku umedumu kuanzia 2020, Kenya ilipokumbwa na janga la Covid-19, japo ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya Corona ulitangazwa kuisha.

Mwaka uliopita, kwenye Makadirio ya Bajeti 2023/2024, Serikali ya Rais William Ruto ilipendekeza nyongeza ya ushuru na ada zinazotozwa bidhaa kutoka nje ya nchi ili kunogesha biashara za ndani kwa ndani.

Sekta ya ufugaji, haswa kuku imeathirika, Rais Ruto akisisitiza kwamba lengo lake ni kuona kilimo kinaimarika kupitia uboreshaji soko la mazao.

Kenya ilikuwa inategemea pakubwa nchi jirani ya Tanzania kupata vifaranga.

Nandi Abisai akilisha kuku wake. PICHA|SAMMY WAWERU

Awali, kifaranga wa siku moja aliyekuwa akigharimu Sh80, bei yake imekwea hadi Sh150.

“Tunahitaji suluhu ya haraka kuangazia kero ya upungufu wa vifaranga,” Abisai akaambia Akilimali Dijitali kupitia mahojiano ya kipekee.

Changamoto hiyo ndiyo imechangia bei ya kuku na mayai kupanda mara dufu.

Mfumko wa bei ya chakula cha madukani, Kevin Kilonzo, mfugaji wa kuku katika Kaunti ya Kiambu na Machakos, pia analia umeathiri wafugaji.

“Kando na vifaranga kuwa ghali, bei ya chakula haikamatiki,” Kilonzo anateta.

Kimsingi, ni changamoto ambazo kwa kiwango kikuu zimechochea mazao ya kuku kuwa ghali.

Kuku kwenye kizimba. PICHA|SAMMY WAWERU

Kuku wa kienyeji aliyeboreshwa aliyekuwa akiuzwa Sh500, sasa hapungui Sh800.

Trei ya mayai ya kawaida – yasiyo na nguvu za uume wa jogoo inachezea Sh450.

Mayai ya kienyeji, moja nalo bei yake imepanda hadi Sh30.