Habari MsetoSiasa

Urafiki wa Uhuru na Joho sasa wanoga

November 13th, 2018 2 min read

Na MOHAMED AHMED

URAFIKI mpya umejitokeza kati ya Rais Uhuru Kenyatta na gavana Hassan Joho. Wawili hao ambao mwaka mmoja uliopita walikuwa kama maji na stima waliporushiana cheche za maneno hadharani, sasa picha zao zimesambaa mitandaoni wakiwa pamoja nchini Ufaransa.

Rais Kenyatta na Bw Joho walikuwa maadui wakubwa kushinda paka na panya, siku chache kabla ya salamu kati ya Rais na kiongozi wa upinzani Raila Odinga mnamo Machi 9.

Katika baadhi ya picha nyengine Bw Joho ameonekana kuandamana na Rais Kenyatta katika mahojiano na wanahabari. Vile vile, Rais Kenyatta alipata fursa ya kutembelea kibanda cha maonyesho cha kaunti ya Mombasa wakati wa kongamano la Amani jijini Paris.

“Rais Kenyatta amesemezana na Wakenya ambao wameweka kibanda chao cha maonyesho katika warsha ya amani ya Paris. Haya yanajiri huku Kenya ikijiandaa kwa warsha yao wiki ijayo,” Ikulu ilisema katika mtandao wa Twitter.

Katika mtandao wake, Bw Joho alisema kuwa maonyesho hayo ni ya kupambana na hamasa kali miongoni mwa vijana.

“Namshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kuja kututembelea katika kibanda chetu na kuzitambua juhudi zetu,” akasema. Akizungumza na Taifa Leo, mkurugenzi wa mawasiliano kaunti ya Mombasa Richard Chacha alisema kuwa kukutana kwa wawili hao ni “sadfa”.

“Lakini kwa sababu wawili hao wamekuwa marafiki wa karibu basi ndio maana wameonekana pamoja. Ukweli ni kwamba viongozi hao wamekuja pamoja kwa ajili ya maendeleo kwa wakazi wa Mombasa na Wakenya kwa jumla,” akasema Bw Chacha.

Kukutana kwa wawili hao huko kunakuja huku Bw Joho mara nyingi akisikika kusisitiza kuwa urafiki wake na Rais Kenyatta upo thabiti kwa sasa.

Bw Joho pia mara kwa mara amerejelea kuwa kushikana kwake na Bw Kenyatta kutaleta manufaa kwa wakazi wake.

Bw Joho amekuwa akiambia wafuasi wake kuwa vita vyake na Rais Kenyatta viliisha na kuwa “mambo yatazidi kubadilika kufuatiya usuhuba huo.”

Gavana huyo pia amesisitiza kuwa atahakikisha kuwa Rais Kenyatta anaafiki ndoto yake ya kuwacha sifa nzuri baada ya kuondoka kwake.

Wiki jana alipokuwa kitui Rais Kenyatta alisisitiza kuwa umoja wa viongozi wote ndio ajenda yake kuu kwa sasa “kwa ajili ya maendeleo ya nchi”.

Kushikana kwa wawili hao kunatia wasiwasi katika kambi ya naibu rais William Ruto ambaye Bw Joho ameapa kupinga juhudi zake za kuwa rais.

Bw Joho kwa upande wake ametangaza kuwa atawania kiti hicho cha urais mwaka 2022, huku wafuasi wake kwenye mitandao wakitazamia usaidizi wa Bw Kenyatta.

Hata hivyo, kuondokewa kwa Bw Joho na baadhi ya wabunge wa kanda hiyo ya Pwani huenda kukazima azma hiyo ya kuwania kiti cha urais wakati wa uchaguzi mkuu ujao.