Michezo

Ureno yazamisha chombo cha Croatia

November 18th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BEKI Ruben Dias wa Manchester City alifunga mabao mawili na kusaidia Ureno kupepeta Croatia 3-2 katika mechi ya UEFA Nations League mnamo Novemba 17, 2020.

Dias alisawazishia Ureno kunako dakika ya 52, sekunde chache baada ya Marko Rog wa Croatia kuonyeshwa kadi nyekundu. Croatia ambao walikuwa wanafainali za Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi walikuwa wa kwanza kuona lango la wapinzani wao katika dakika ya 29 kupitia kwa Mateo Kovacic wa Chelsea.

Ingawa Joao Felix wa Atletico Madrid alisawazishia Ureno katika dakika ya 60, Kovacic alifunga tena kabla ya Ureno kuzoa ushindi kupitia kwa Dias.

Ushindi wa 4-2 uliosajiliwa na Ufaransa dhidi ya Uswidi kwenye mechi nyingine ya Kundi A3 uliwaepushia Croatia shoka ambalo vinginevyo lingaliwashusha ngazi hadi League B.

Ushindi uliosajiliwa na Ufaransa dhidi ya Ureno mnamo Novemba 14 ulizamisha kabisa matumaini ya mabingwa watetezi Ureno kufuzu kwa fainali za Nations League mwaka huu baada ya kutawazwa wafalme mnamo Juni 2019.

Licha ya kujivunia huduma za nyota Cristiano Ronaldo, Diogo Jota na Bruno Fernandes, kikosi cha Ureno hakikung’aa dhidi ya Croatia jinsi ilivyotarajiwa.

Masihara ya beki Ruben Semedo katika dakika ya 29 yalimpa fowadi Mario Pasalic fursa ya kumwandalia Kovacic krosi safi kabla ya nyota huyo wa Chelsea kumtatiza sana kipa Rui Patricio.