Habari Mseto

Urithi Housing yaahidi mazuri upande wa makazi

May 31st, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

CHAMA cha Ushirika cha Urithi Housing Cooperative Ltd na kampuni ya ujenzi ya Meera Construction, wanaendelea na ujenzi na uuzaji wa majumba ili kuafikia mojawapo ya ajenda nne muhimu za serikali ya Jubilee.

Kulingana na Mwenyekiti wa chama cha Urithi, Bw Samuel Maina, nyumba hizo zilizoko katika eneo la Green Zone Estate, ni pamoja na majumba yenye vyumba vya kulala idadi ya 283 katika makazi ya Serena, Thindigua katika barabara kuu ya Kiambu; kilomita chache kutoka UN Avenue.

Bw Maina alisema mazingira katika eneo hilo ni ya kuridhisha ambapo kina eneo kubwa la kuegesha magari na sehemu kubwa ya kufanya ujenzi zaidi.

“Lengo letu kuu ni kuona ya kwamba ajenda nne za serikali zinaafikiwa hasa kwa ujenzi wa majumba ya makazi. Tuko mbioni kuona ya kwamba ifikapo mwaka wa 2022 tutakuwa na jambo la kujivunia,” alisema Bw Maina.

Alisema eneo la Green Zone Estate liko mkabala wa dukakuu la Quick Mart Supermarket na liko karibu na kituo cha biashara, likiwa pia karibu na shule za kifahari na barabara kuu.

Kulingana na Maina, nyumba zitakazojengwa eneo hilo ni za kisasa ambapo zitavutia watu wengi wenye nia ya kuzinunua.

Baadhi ya nyumba zinazojengwa eneo hilo ni zenye mandhari ya kupendeza. Kila moja ina vyumba vya kulala viwili. Hizo ni jumla ya majumba 64.

Kuna zingine za vyumba vya kulala vitatu. Jumla yazo ni majumba 160.

Kwenye nyumba hizo kuna jikoni za kifahari zenye mitambo ya kupikia chakula na vifaa vya umeme; ovena na microwave.

Mfano wa majumba ya ghorofa yanayotarajiwa kujengwa na kuuzwa kwa wanachama na watu wenye nia ya kumiliki nyumba zao wenyewe. Picha/ Hisani

Kila eneo ambapo panajengwa majumba hayo kuna maegesho. Nako ndani ya majumba kuna eneo la kuunganisha umeme kwa kutumia runinga na mtandao wa Intaneti.

Bw Maina alieleza uzuri wa ujenzi huo kwa sababu kutakuwa na ulinzi wa saa 24 huku kukiwa na ukuta uliotundikwa umeme ili kuzuia wizi na uhalifu wakati wowote.

Alisema majumba ya ghorofa yatawekwa lifti zitakazobeba wakazi wanaoishi juu kabisa.

Nyumba hizo pia zitakuwa na maji moto kila chumba huku maji ya visima yaikiwekwa kila eneo ili kusaidia wakati kuna upungufu wa maji.

Katika maeneo hayo kutakuwepo na mabwawa ya kuogelea; swimming pools na maeneo ya kufanyia mazoezi; gym kwa wanaotaka kunyoosha viungo vyao.

Pia kutakuwepo na kamera za siri; CCTV, kurekodi matukio kwa sababu za usalama. Pia kutakuwa na ukumbi mkubwa wa kusaidia wakazi kuendeleza maswala yao ya kibinafsi na michezo kadha.

Bw Maina alisema awamu ya kwanza ya nyumba za vyumba viwili na vitatu itakamilika ifikapo Aprili 2020. Halafu zilizosalia zitakuwa tayari ifikapo Desemba 2020.