Urithi wa Raila wagawa ODM

Urithi wa Raila wagawa ODM

RUSHDIE OUDIA na BENSON MATHEKA

KAMPENI za chini kwa chini za kumrithi kiongozi wa ODM Raila Odinga kama msemaji wa eneo la Nyanza, zimewagawanya washirika wake wa kisiasa.

Mgawanyiko huo ulipanuka jana baada ya kundi linaloongozwa na wabunge Junet Mohamed (Suna Mashariki) na John Mbadi (Suba) kumuondoa Mbunge wa Rarienda, Otiende Amollo kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Sheria.

Bw Amollo amekuwa kwenye kundi pinzani linaloongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo, na nafasi yake sasa imechukuliwa na Mbunge wa Ruaraka, TJ Kajwang.

Makundi matatu yanang’ang’ana kumrithi Bw Odinga baada ya kuibuka kuwa huenda akaamua kutowania urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Makundi hayo ni ya mrengo unaopigania uongozi wa wanasiasa vijana kutoka Nyanza, wanaohisi kwamba kuna haja ya damu mpya miongoni mwa viongozi wanaomzunguka Bw Odinga, ambao duru zinasema wanapanga kuwaondoa wale ambao wamekuwa washirika wake kwa muda mrefu.

Mrengo huo unajumuisha Bw Mbadi, Bw Junet, Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi na aliyekuwa mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo.

Kundi la pili linahusisha wanaotetea wakongwe ambao wamemzingira Bw Odinga kwa miaka mingi. Hawa wanaongozwa na Bw Orengo na Bw Amollo wakishirikiana na wabunge Samuel Atandi (Alego Usonga), Peter Kaluma (Homa Bay Mjini) na Millie Odhiambo wa Suba Kaskazini.

Kundi la tatu linaongozwa na Gavana wa Migori, Zachary Obado ambaye anaamini wakazi wa Nyanza wanahitaji mwelekeo mpya wa kisiasa baada ya Bw Odinga kuondoka ulingoni.

Bw Odinga hajazungumzia mgawanyiko wa washirika wake, lakini mkutano wake majuzi na Bw Wandayi na Bw Junet nyumbani kwake unaonyesha kwamba anaelewa hali inayokumba ngome yake.

VIATU VYA RAILA

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanasema kwamba itakuwa vigumu kwa wanasiasa hao kutoshea katika viatu vya Bw Odinga, ambaye amehimili mawimbi ya kisiasa kwa miaka mingi.

“Raila anapoelekea kukamilisha safari yake kama baba wa siasa za Nyanza, viongozi wengi wa jamii ya Waluo watamzunguka wakitaka kutawazwa kuwa mrithi wake. Lakini hakuna kati yao aliye na ari, nia na nguvu za kuvaa viatu vyake,” asema mchanganuzi Alhaji Amin.

Anasema japo Bw Orengo na Gavana wa Kisumu, Anyang’ Nyongo wamekuwa wandani wa Bw Odinga kwa miaka mingi, umri umewaandamana sawa na waziri mkuu huyo wa zamani.

Anasema wanachofaa kufanya wanasiasa wanaotaka kumrithi ni kumsaidia kutimiza ndoto yake ya kuwa rais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Suala la kampeni za kumrithi Bw Odinga limekuwa kiazi moto hivi kwamba hakuna anayetaka kuligusia, huku waliopigiwa simu na waandishi wetu wakikataa kuzijibu na wale waliojibu wakiomba kutolizungumzia kwa wakati huu.

KUMLAZIMISHA KUSTAAFU

Mwanasiasa mmoja mwandani wa Bw Odinga alithibitisha kwamba kuna kampeni za kurithi Bw Odinga.

Kulingana na Bw Midiwo, kuna vita vya mapema vya kumrithi Bw Odinga ambapo viongozi tofauti wanataka kuwa vinara wa jamii ya Waluo eneo la Nyanza.

“Hatutakubali yeyote anayetaka kumlazimisha Raila astaafu siasa mapema. Tunawajua na hatutakubali,” alisema Bw Midiwo akiongea na kituo kimoja cha redio.

Kuchacha kwa mzozo baina ya makundi hayo kumevutia Baraza la Wazee wa Waluo, ambao wanahofia kwamba unaweza kuathiri mchakato wa BBI na azma ya urais ya Bw Odinga.

Kulingana na Mzee Odungi Randa, ambaye ni mwanachama wa baraza hilo, wataita mkutano wa viongozi wote ili kutuliza mgawanyiko huo kabla haujavuruga mambo zaidi.

You can share this post!

Suluhu asaidia kusuluhisha matatizo kati ya Wakenya na...

NEMA: Walionyakua ardhi ufuoni na sehemu ya bahari waonywa...