HabariSiasa

UROHO: Matumbo ya wabunge yasiyoshiba

June 6th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE na maseneta wanakutana Alhamisi kujadili mbinu za kuiadhibu Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya watumishi wa umma (SRC), kwa kupinga hatua yao kulipwa marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi.

Kikao hicho kisicho rasmi, almaarufu, ‘Kamukunji’, kiliitishwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kufuatia ombi lililowasilishwa na Mbunge wa Homa Bay Mjini, Peter Kaluma.

Mnamo Ijumaa iliyopita, Mahakama Kuu iliamuru Tume ya Huduma za Bunge (PSC) isitishe kuwalipa wabunge marupurupu ya nyumba hadi kesi iliyowasilishwa na SRC kupinga malipo hayo itakaposikizwa na kuamuliwa.

SRC inayoongozwa na Bi Lyn Mengich inataka mahakama kuwaamuru wabunge warejeshe pesa ambazo tayari wamepokea kama marupurupu ya nyumba, ikisema PSC ililipa pesa hizo kinyume cha sheria.

Ikiwa tume itafaulu, wabunge na maseneta 416 watalazimika kurejesha Sh2.21 milioni ambazo kila mmoja wao alipokea mwishoni mwa Aprili ikiwa ni malimbikizi ya tangu mwezi Oktoba 2018.

Kuishtaki SRC

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba wabunge na maseneta wananuia kutumia mkutano huo kupanga mikakati ya kuishtaki SRC kwa kutumia Sh99 milioni kununua magari ya kifahari bila idhini ya Bunge, kama njia ya kuiadhibu tume hiyo kwa kuzuia walipwe marupurupu.

Tayari Kamati ya Bunge kuhusu Fedha imekataa kuidhinisha matumizi ya fedha hizo kwa mujibu wa kipengee cha 223 kinachoziruhusu asasi za umma kutumia fedha katika shughuli za dharura hata kabla ya kupata idhini ya Bunge.

“Hawa watu wa SRC ni wanafiki. Mbona wanadai eti wabunge ni walafi ilhali wao wanatumia pesa za umma kujinunulia magari ya kifahari bila kufuata sheria?,” akauliza Mbunge wa Alego Usonga, Samuel Atandi.

Mnamo Jumanne, Spika Muturi alisema aliwaalika wabunge kwa mkutano huo ili kutoa nafasi kwao kufahamishwa kuhusu vuta nikuvute inayoendelea kati ya SRC na PSC.

“Bw Kaluma alikuwa ameibua mambo muhimu katika barua yake kwa Spika na kutupa fursa kujadili masuala hayo katika mkutano wa Alhamisi saa tano. Maseneta pia watahudhuria,” akasema Bw Muturi ambaye ndiye mwenyekiti wa PSC.

Swali kuu

Naye Bw Kaluma alisema wanapanga kuibua maswali kuhusu mishahara mikubwa ambayo makamishna wa SRC hupokea, marupurupu ya nyumba na yale ya vikao.

“Mbona wao wanapokea mishahara ya Sh1 milioni kila mwezi, marupurupu ya nyumba ya Sh320,000 na Sh50,000 za kila kikao ilhali hatawataki wabunge kupokea Sh250,000 za nyumba?” akauliza.

Hata hivyo, uchunguzi wetu ulibaini kuwa ni mwenyekiti wa SRC pekee ambaye hupokea mshahara wa Sh1,082, 528 huku makamishna wengine wakipata Sh717,568 kila mwezi.

Tayari Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti imepunguza mgao wa fedha kwa SRC katika bajeti itakayosomwa mwezi huu kwa Sh104 milioni, hatua inayoonekana kama ya kuiadhibu tume hiyo.

Kando na hayo wabunge wamepinga ombi la SRC la kutaka itengewe Sh300 milioni za kujenga afisi mpya.

“Hakuna haja kwa SRC kuitisha pesa za kujenga afisi mpya ilhali kuna majengo mengi ya serikali ambayo wanaweza kutumia,” akasema Bw John Mbadi ambaye ni kiongozi wa wachache bungeni.