KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uruguay na Korea Kusini watoshana nguvu kwa sare tasa katika gozi la Kundi H ugani Education City

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uruguay na Korea Kusini watoshana nguvu kwa sare tasa katika gozi la Kundi H ugani Education City

Na MASHIRIKA

URUGUAY na Korea Kusini waliambulia sare tasa ugani Education City katika mchuano wao wa ufunguzi wa Kundi H kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar.

Korea Kusini walihanganisha Uruguay japo wenyewe hawakupata fursa nyingi za kufunga mabao. Nafasi nzuri zaidi waliyoipata ni kupitia kwa Hwang Ui-jo aliyepaisha kombora lake kabla ya nahodha wa Uruguay, Diego Godin, kushuhudia mpira alioupiga kwa kichwa ukibusu mhimili wa lango la wapinzani.

Licha ya Korea Kusini kudhibiti dakika za mwanzo za mechi hiyo, Uruguay walitamalaki asilimia kubwa ya mpira na nusura wafunge bao mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa Federico Valverde.

Fowadi mahiri wa Tottenham Hotspur, Son Heung-min, naye alipoteza nafasi kadhaa za wazi za kufungia Korea Kusini mwishoni mwa kipindi cha pili.

Matokeo hayo yanaacha Kundi H kuwa wazi kwa yeyote kufuzu kati ya Uruguay, Korea Kusini na Ureno wanaoongozwa na kigogo Cristiano Ronaldo. Ghana ambao wana kikosi cha chipukizi wengi zaidi kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, pia wako katika Kundi H.

Huku Korea Kusini wakimtegemea zaidi maarifa ya Son, Uruguay ambao ni mabingwa mara mbili wa Kombe la Dunia (1930, 1950) wanajivunia huduma za nyota Darwin Nunez, Luis Suarez na Edinson Cavani.

Mechi kati ya Uruguay na Korea Kusini ilikuwa ya tatu kukamilika kwa sare tasa kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu baada ya matokeo sawa na hayo kusajiliwa na Tunisia dhidi ya Denmark katika Kundi D kabla ya Morocco pia kulazimishia Croatia sare tasa katika Kundi F.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Raila ahudhuria kikao cha kukaanga Cherera na wenzake kisha...

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ronaldo aweka rekodi mpya ya...

T L