Michezo

URUSI 2018: Ahadi ya pesa ilivyochochea Nigeria kuiyeyusha Iceland

June 25th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

SUPER Eagles ya Nigeria ilipata msukumo wa kudhalilisha Iceland kutokana na ahadi ya Sh5,045,225 (Naira 18 milioni) kwa kila bao kutoka kwa wadhamini, Aiteo Group.

Taarifa nchini Nigeria zinasema vijana wa kocha Gernot Rohr watapata zawadi hiyo tu wakishinda mpinzani bila kufungwa bao. Ina maana kwamba kwa kunyuka Iceland 2-0 Juni 22 kwenye Kombe la Dunia linaloendelea nchini Urusi, Super Eagles ilitia kibindoni Sh10,090,450.

Katika mchuano huo wa Kundi D, mshambuliaji Leicester City Ahmed Musa, ambaye yuko CSKA Moscow kwa mkopo, alitikisa nyavu za Iceland mara mbili.

Nigeria haikuwa na shuti hata moja lililenga goli katika kipindi cha kwanza kabla ya Musa kufanga mabao haya safi katika dakika ya 49 na 75. Mabingwa hawa mara tatu wa Afrika waliingia mechi ya Iceland wakiuguza kichapo kikali cha mabao 2-0 walichopokea kutoka kwa Croatia mnamo Juni 17.

Nigeria inashikilia nafasi ya pili kwa alama tatu, tatu nyuma ya viongozi Croatia. Vijana wa Rohr watakamilisha mechi za makundi dhidi ya Argentina mnamo Juni 26.