HabariMichezo

URUSI 2018: Mastaa watakaonogesha dimba

June 13th, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WAKATI kipenga cha kuashiria mwanzo wa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi kitakapopulizwa rasmi Alhamisi, wadadisi wa soka wanahisi kwamba ladha ya kivumbi cha mwaka huu itakolezwa zaidi na masogora ambao huenda fainali hizi ziwe zao za mwisho kushiriki.

Kulingana na vyombo vingi vya habari, wachezaji Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Andres Iniesta, David Silva na wengineo ni baadhi ya watakaopania kustaafu soka ya kimataifa kwa matao ya juu na hivyo, watatawaliwa na kiu ya kutambisha vikosi vyao nchini Urusi.

 

CRISTIANO RONALDO

Nyota huyo wa Real Madrid ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Ureno (mabao 81) baada ya kuvalia jezi za timu ya taifa katika jumla ya michuano 149 iliyopita.

Baada ya kuwaongoza Man-United na Real kutia kapuni ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza, Uhispania na Klabu Bingwa Ulaya na Klabu Bingwa Duniani, taji la pekee la haiba kubwa ambao Ronaldo hajanyanyua wakati akivalia jezi za timu ya taifa ni Kombe la Dunia.

Mnamo 2016, Ronaldo aliwachochea Ureno kutawazwa mabingwa wa Euro 2016 nchini Ufaransa.

Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa taji la Ballon d’Or ambalo hutolewa kwa Mchezaji Bora Duniani kila mwaka, aliwafungia Ureno bao muhimu kwenye fainali za Kombe la Dunia mnamo 2006 nchini Ujerumani kabla ya kufanya hivyo kwa mara nyingine mnamo 2010 na 2014 nchini Afrika Kusini na Brazil mtawalia.

Baada ya Ureno kufungua kampeni za Kundi B dhidi ya mabingwa wa 2010 Uhispania mnamo Juni 15, kikosi hicho kitamenyana na Morocco mnamo Juni 20 kabla ya kupepetana na Iran siku tano baadaye.

 

LIONEL MESSI

Mfumaji huyo matata wa Barcelona atategemewa na kocha Jorge Sampaoli kuyaweka hai matumaini ya mashabiki wa Argentina kadri atakavyojitahidi kushirikiana na wavamizi Sergio Aguero, Angel Di Maria, Paulo Dybala na Gonzalo Higuain.

Messi ambaye ametawazwa mwanasoka bora duniani mara tano, hajashinda taji lolote muhimu akivalia jezi za Argentina hasa ikizingatiwa kwamba walizidiwa na Ujerumani kwenye fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2014 kabla ya Chile kuwapiga kumbo katika Copa America mnamo 2015 na 2016 mtawalia.

Japo amekuwa akikosolewa na kulaumiwa pakubwa kwa madai ya kutojituma kwa asilimia 100 kila anapowachezea Argentina, Messi anatarajiwa akuduwaza wengi nchini Urusi. Argentina wamepangwa pamoja na Iceland, Croatia na Nigeria katika Kundi D.

 

ANDRES INIESTA

Nguli huyo wa soka aliagana rasmi na Barcelona mwishoni mwa msimu huu na kutia saini mkataba na Vissel Kobe ya Japan. Iniesta alibanduka Barcelona baada ya kuvalia jezi za miamba hao wa La Liga zaidi ya mara 670 katika kipindi cha misimu 16.Ushawishi wa nahodha huyo wa Barcelona ulimwezesha kutia kibindoni jumla ya mataji 31 katika ngazi ya klabu na makombe matatu akiwasakatia Uhispania ambao wanapigiwa upatu wa kutamba kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka huu.

Awali, vyombo vingi vya habari ndani na nje ya Uhispania vilimhusisha Iniesta na uwezekano mkubwa wa kutua Uingereza kwa nia ya kuisakatia Manchester City ya kocha Pep Guardiola.

Chini ya unahodha wa Iniesta, Uhispania walitia kapuni ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2010, Euro 2008 na Euro 2012.

Wachezaji wengine wanaotazamiwa kutambisha pakubwa vikosi vyao ni Mohamed Salah (Misri), Edinson Cavani, Luis Suarez (wote Uruguay), Diego Costa (Uhispania), Antoine Griezmann, Kylian Mbappe (Ufaransa), Paulo Dybala, Aguero (wote Argentina), Thomas Muller (Ujerumani), Romelu Lukaku, Eden Hazard (Ubelgiji), Harry Kane, Raheem Sterling (Uingereza), Robert Lewandowski (Poland) na Sadio Mane (Senegal).