Kimataifa

Urusi yaendelea kuponda Ukraine kwa makombora; yaua watu 20 zaidi hospitalini

Na MASHIRIKA July 8th, 2024 2 min read

KYIV, UKRAINE

TAKRIBAN watu 20 wafariki baada ya wanajeshi wa Urusi kurusha makombora zaidi ya 40 katika hospitali moja ya watoto jijini Kyiv na miji mingine nchini Ukraine.

Katika tukio hilo lililofanyika Jumatatu mchana, uharibifu mkubwa wa miundombinu, ikiwa ni pamoja na hospitali hiyo ulishuhudiwa.

Shambulio hilo lilitokea wakati kiongozi wa Hungary, Victor Orban alipotembelea Rais Xi Jinping wa China kujadili mikakati ya kufanywa ili kuafiki makubaliano ya kurejesha amani.

Taarifa zaidi zilieleza kwamba Urusi ilirusha msururu wa makombora katika mji wa Kyiv na miji mingine ya Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alisema vikosi vya Urusi vilirusha makombora zaidi ya 40 vikilenga miji tofauti na kuharibu miundombinu, majengo ya biashara na makazi katika miji tofauti ya Ukraine.

Maafisa wa serikali katika jiji la Kyiv walisema watu saba waliuawa na wengine 25 kujeruhiwa katika jiji hilo kuu la Ukraine.

Kadhalika, katika eneo la Kryviy Rih, mji wa asili wa Zelenskiy, watu 10 waliuawa na wengine 31 kujeruhiwa, Meya wa mji huo, Oleksandr Vilkul alisema.

Kulingana na gavana wa mkoa wa Donestk, watu wengine watatu walifariki katika eneo la Pokrovsk Mashariki mwa Ukraine wakati makombora yalipopiga kituo cha viwanda.

Rais Zelensky aomba msaada kutoka kwa jamii ya kimataifa

Kwenye programu ya ujumbe wa Telegraph, Zelensky alisema: “Juhudi zote zinafanywa kuokoa watu wengi iwezekanavyo. Dunia nzima inapaswa kufanya liwezekanalo ili kukomesha vita vya Urusi.”

Urusi imekanusha mara kwa mara kuwalenga raia wakati wa mashambulio yake.

Mashambulio makubwa dhidi ya Ukraine yalijiri wakati Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban alikuwa na kikao na Rais wa China Xi Jinping.

Katika mkutano huo, wawili hao walijadiliana kuhusu makubaliano ya kufanya mikakati ya Ukraine kusitisha vita, wakati Orban alipoitembelea Uchina.

Vilevile, Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko alisema shambulio dhidi ya Kyiv lilikuwa moja ya mashambulio mazito zaidi tangu Urusi ianze kuishambulia nchi ya Ukraine mnamo Februari mwaka 2022.

Alisema hospitali kuu ya watoto mjini humo iliharibiwa katika tukio hilo.

Madirisha yalivunjwa na fremu kung’olewa. Wazazi waliokuwa wamebeba watoto wachanga walitoka nje barabarani wakiwa wameduwaa na kulia.

“Tulisikia mlipuko, kisha tukamwagikiwa na vifusi,” Svitlaka Kravchenko, 33, aliambia shirika la habari la Reuters baada ya yeye na mumewe Viktor, kujitokeza barabarani.

Mtoto wao wa miezi miwili hakujeruhiwa, lakini Svitlana alijeruhiwa, na gari lao lilizikwa kabisa na vifusi vya jengo lililoharibiwa katika ua kutoka kwa wadi kuu.

Mwathiriwa Viktor alisema, “Sikuweza kupumua, nilijaribu kufunika mtoto wangu kwa kitambaa hiki ili aweze kupumua”.

Serikali ilisema kwamba viwanda, miundombinu na majengo ya makazi na biashara yaliharibiwa katika miji ya Kyi, Kryviy Rih, Dnipro, Pokrovsk, Kramatarosk na maeneo mengine mbalimbali.