Urusi yalemewa kulipa madeni yake ya kigeni

Urusi yalemewa kulipa madeni yake ya kigeni

NA MASHIRIKA

NEW YORK, AMERIKA

URUSI imeshindwa kulipa deni lake la kitaifa kwa mara ya kwanza katika karne moja iliyopita.

Hali imetajwa kuchangiwa na vikwazo vingi vya kifedha ilivyowekewa na mataifa ya Magharibi.

Taifa hilo liliwekewa faini nyingi kwa madeni lililo nayo, kutokana na hatua yake kuivamia Ukraine mnamo Februari mwaka huu.

Urusi ilikuwa imepewa hadi Jumapili kulipa riba ya Sh1 bilioni kwa madeni inayodaiwa. Hii ni baada ya muda rasmi iliyokuwa imepewa kuisha Mei 27.

Hata hivyo, muda huo ulipita bila Urusi kulipa fedha hizo wala serikali ya Rais Vladimir Putin kutoa taarifa yoyote.

Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wanataja hilo kuwa “doa” kubwa, kwani hilo linaachilia Urusi inaendelea kutengwa kiuchumi, kifedha na kisiasa na mataifa mengine duniani.

Tangu kuivamia Ukraine mnamo Februari, hisa za mashirika tofauti zimekuwa zikishuka bei, huku akaunti nyingi za kigeni za benki yake kuu zikifungwa.

Benki kubwa nchini humo pia zimeondolewa kwenye mfumo wa kifedha unaoziunganisha benki zote duniani.

Wataalamu wanasema huenda hali hiyo ikakosa kuwashangaza raia wengi wa taifa hilo, kwani wamekuwa wakikabiliwa na gharama ya juu ya maisha tangu vita hivyo kuanza.

Bei za bidhaa za msingi zimekuwa zikipanda sana, huku hali ya uchumi wa taifa hilo ukielezwa kuwa katika hali mbaya, ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa miaka mingi.

Hata hivyo, Urusi inasisitiza kuwa ina fedha za kutosha kulipa madeni yake na wiki iliyopita ilisema italipa deni lake la Sh4 trilioni kwa sarafu zake.

“Taswira ya kuwa tumeshindwa kulipa deni letu imebuniwa na mataifa ya Magharibi. Yanatuwekea masharti ambayo tutazingatia katika kulipa deni hilo. Tutalipa kwa sarafu yetu,” ikasema taarifa kutoka kwa serikali.

“Ni nadra sana kwa serikali ambayo ina uwezo wa kulipa madeni yake kulazimishwa na serikali za kigeni,” akasema Hassan Malik, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha katika shirika la kifedha la Loomis Sayles and Company LP, lenye makao yake jijini New York, Amerika.

Ijapokuwa taarifa rasmi za nchi kushindwa kulipa deni lake huwa zinatolewa na mashirika makubwa ya kifedha baada ya kufanya utathmini kwa taifa husika, mashirika hayo yaliacha kufuatilia hali ya kiuchumi nchini Urusi ilipoanza uvamizi wake dhidi ya Ukraine.

Wataalamu wanasema kile kitakachofuata baada ya hilo ni mwelekeo ambao wawekezaji nchini humo watachukua.

“Huenda wakakosa kuchukua maamuzi ya haraka. Wanaweza kuamua kutathmni mwelekeo wa vita hivyo kwa matumaini kuwa huenda baadhi ya vikwazo hivyo vikapunguzwa,” akaeleza mtaalamu huyo.

Wakati huo huo, Urusi iliendeleza mashambulio yake dhidi ya Ukraine, licha ya kongamalo la mataifa wanachama wa muungano wa G7 kuendelea nchini Ujerumani.

Jiji kuu, Kyiv, ndilo lililorushiwa makombora mengi kwenye mashambulio hayo.

Maafisa wa serikali walisema kuwa jengo moja kubwa liliharibiwa huku mtu mmoja akifariki.

Ukraine ilisema jumla ya makombora 14 yalirushwa katika jiji hilo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Tuchukue tahadhari kuepusha hatari katika kampeni

Afueni ya bei ya mafuta yanukia Agosti

T L