Urusi yashutumiwa kwa ‘kulinda’ waasi

Urusi yashutumiwa kwa ‘kulinda’ waasi

Na AFP

UMOJA WA MATAIFA, Amerika

AMERIKA, na mataifa washirika wake, yameishutumu Urusi kwa kutambua uhuru wa maeneo yaliyokaliwa na waasi nchini Ukraine na kuwapeleka wanajeshi wa kulinda amani katika maeneo hayo.

Akiongea katika kikao cha dharura cha Baraza la Amani la Umoja wa Mataifa (UNSC), Balozi wa Amerika Linda Thomas-Greenfield, alisema ni kitendo cha ukiukaji wa sheria ya kimataifa kwa Urusi kuyatambua maeneo ya Donetsk na Lugansk na kuyaweka chini ya ulinzi wa majeshi yake.

Thomas-Greenfield pia alitaja hatua hiyo kama “kisingizio” cha Rais wa Urusi Vladimir Putin cha kutaka kuanzisha vita na Ukraine, ishara kwamba mzozo kati ya nchi hizo mbili hautakoma hivi karibuni.

“Eti anawaita wanajeshi wa kulinda amani. Huu ni upuzi. Tunafahamu na tunajua malengo yao,” balozi huyo akasema.

Balozi wa Ukraine Sergiy Kyslytsya, ambaye pia alihudhuria mkutano huo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) Jumatatu, alisisitiza kuwa mipaka ya nchi ya nchini yake haitabadilishwa licha ya vitendo vya Urusi.

Huku hayo yakijiri, Balozi wa Urusi katika UN Vasily Nebenzya, alisema nchi yake ingali tayari kusuluhisha mzozo huo kwa “njia ya kidiplomasia”.

Hata hivyo, alionya dhidi ya kile alichokitaja kama “uchokozi wa Ukraine”.

“Hatungetaka umwagikaji wa damu utokee katika Donbass,” akaongeza akirejelea eneo pana linalojumuisha maeneo ya Donetsk na Lugansk.

Amri ya Rais Putin inafasiriwa kama inayolenga kutoa nafasi ya kupelekwa kwa wanajeshi wengi kwenye mpaka katika ya Urusi na Ukraine.

Kwenye hotuba ndefu kwa taifa iliyopeperushwa kupitia runinga, aliyotoa akitangaza kutambuliwa kwa maeneo yanayodhibitiwa na waasi, Putin alishutumu Ukraine akiitaja kama “kikaragosi” cha mataifa ya magharibi.

Aliitaja kama taifa “lililofeli” na ambalo zamani lilikuwa sehemu ya Urusi.

Lakini kwa upande wake balozi Thomas-Greenfield alitaja hotuba hiyo kama iliyosheheni madai ya uwongo ambayo yanalenga “kutoa kisingizio cha kuanza kwa vita”.

Kauli ya balozi huyo wa Amerika ilijiri kabla ya msemaji mmoja wa Ikulu ya White House kuambia AFP kwamba Amerika itaiwekea Urusi vikwazo kutokana na amri ya Putin.

Urusi, ambayo wakati huu inashikilia kiti cha urais wa baraza la UNSC, awali ilitaka kikao cha Jumatatu jioni kuwa cha faragha lakini Amerika ikasisitiza kiwe wazi.

Mataifa kadha yalikuwa yameitisha mkutano huo wa dharura kwa misingi ya barua kutoka kwa Ukraine iliyoomba kwamba mwakilishi wake aweze kuhudhuria.

Akiongea Jumatatu jioni, Kyslytsya, aliitaka baraza hilo la usalama la UN kupuuzilia mbali vitisho kutoka kwa Urusi.

Akasema: “Wanachama wa UN wasiruhusu kuambukizwa virusi vinavyoenezwa na Urusi. UN isikubali kuambukizwa ugonjwa huu.”

Katibu anayesimamia masuala ya Siasa na Amani katika UNSC Rosemary DiCarlo, alisema ni jambo la “kusikitisha” kwamba wanajeshi wa Urusi walipelekwa mashariki mwa Ukraine.

“Saa na siku zijazo zitakuwa zenye umuhimu mkubwa zaidi kuhusiana na mzozo huu,” DiCarlo akasema.

“Kuna hatari ya kutokea kwa vita vikubwa na hatari hiyo inafaa kudhibitiwa kwa njia zozote zile,” akaongeza.

Balozi wa Uingereza Barbara Woodward, alisema wanachama wa UNSC wanafaa kuungana katika kuhimiza Urusi kukomesha vitendo vinavyoweza kuchochea vita kati yake na Ukraine.

Mabalozi wengine walioshutumu Urusi katika kikao hicho cha Jumatatu ni; Geraldine Byrne Nason (Ireland) na Martin Kimani (Kenya).

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Smoker itakusaidia kukaribia mzinga na kuvuna...

TAHARIRI: Serikali ikabili mfumko wa bei za bidhaa kuokoa...

T L