Habari

Usahihishaji wa KCSE kufanyika kwa wiki mbili

December 1st, 2019 1 min read

NA OUMA WANZALA

WALIMU zaidi ya elfu 26 wameanza kusahihisha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne(KCSE) uliokamilika wiki iliyopita.

Shughuli hiyo inafanyika katika vituo 20 jijini Nairobi na viungani mwake.Mchakato huo wa usahihishaji unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha majuma mawili yajayo.

Usahihishaji huo ulianza rasmi Jumamosi na unafanyika kila siku kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tano usiku.

Wakuu wa kitengo cha usahihishaji na washirikishaji walikuwa wamekita kambi jijini Nairobi wiki jana ili kufanya maandalizi kabambe kuhusu namna ya kuendesha shughuli hiyo ya majuma mawili.

Kwanza, walimu wasahihishaji walilazimika kufanya mtihani huo ili kupima kiwango cha uelewaji pana wa masomo watakayowajibikia.

Kulingana na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, usahihishaji huo unatarajiwa kuwa na viwango vya juu vya umakinifu kwa kuwa hakuna mwalimu atakayeruhusiwa kusahihisha zaidi ya swali moja kwenye somo husika.

“Tunatilia manani sana ukamilishaji wa shughuli hii kwa wakati kabla ya sherehe za Krismasi,” akasema Prof Magoha akiongeza kwamba wataalamu wa teknolojia watatekeleza jukumu muhimu wakati wa usahihishaji huo.

Wakati wa usahihishaji, walimu huwekwa kwenye matapo saba huku kila tapo likiwa na kiongozi wake.

Kwa kila karatasi 10 ambazo husahihishwa, kiongozi huyo huchagua karatasi mbili na kuangalia iwapo zimesahihishwa kwa njia ya kitaalamu na alama sahihi kutunukiwa mtahiniwa.

Mtihani wa KCSE ulianza Novemba 4 na kukamilika Novemba 27.