Habari

Usajili: Agizo la Rais lafanya wengi kulegea

May 18th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAKENYA wamelegeza bidii ya kupokea Huduma Namba baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuamuru muda wa kujisajili uongezwe kwa siku saba zaidi.

Foleni zilikuwa fupi Jumamosi katika vituo vya usajili ambavyo Ijumaa vilikuwa na idadi kubwa ya watu kupita kiasi waliotarajia siku ya mwisho ya usajili ingekuwa jana kama ilivyopangwa awali.

Baadhi ya watu walikosa kwenda kazini siku hiyo, watoto nao wakikosa kuhudhuria masomo kusudi waende kusajiliwa kabla ya siku ya mwisho ambayo ilikuwa jana, Mei 18, 2019.

“Rais amefanya vizuri kuongeza muda wa usajili kwa wiki moja. Sasa mimi nitaenda kusajiliwa Jumanne wiki ujao,” akasema mwanamume mmoja ambaye huuza peremende katika kituo cha mabasi cha Kencom, katikati mwa jiji la Nairobi.

Kwenye hotuba aliyotoa katika Ikulu ya Nairobi Ijumaa jioni, Rais Kenyatta alitoa amri ya kuongezwa kwa muda huo wa usajili baada ya kushuhudia foleni ndefu za Wakenya waliojitokeza kwa shughuli hiyo siku za mwisho.

“Nimeangalia na kuona foleni ndefu wakati wa siku hizi za mwisho za shughuli hii katika sehemu mbalimbali nchini. Hii inadhihirisha tabia yetu ya kushughulikia mambo saa za mwisho jambo ambalo limeendelea kutuzuia kupiga hatua. Hata hivyo, inaridhisha kuwa Wakenya wamejitolea kujisajili kupata Huduma Namba na nimekubali maombi yao ya kuwapa muda zaidi kufanya hivyo,” akaeleza.

“Hivyo basi naiagiza kamati inayohusika na utekelezaji mpango huu, kuongeza muda wa usajili kwa wiki moja. Hii ina maana kuwa zoezi hili litakamilika mnamo siku ya Jumamosi ijayo Mei, 25 saa kumi na mbili jioni,” Rais Kenyatta akasisitiza.

Kiongozi wa taifa aliwahimiza wale ambao hawajajisajili kutumia kikamilifu muda huu wa ziada wajisajili badala ya kusubiri hadi siku ya mwisho.

Wakati uo huo kiongozi wa taifa alisema kuwa usajili wa Wakenya wanaoishi ughaibuni ulioanza Mei 6 katika balozi za Kenya utaendelea hadi Juni 20, 2019.