Habari

Usajili wa makurutu wa KDF kuanza Novemba 27

October 28th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SHUGHULI ya kuwasajili makurutu wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) sasa itaanza Novemba 27, kwa mujibu wa makao makuu ya Wizara ya Ulinzi.

Na wale ambao walikuwa wametuma maombi wali wameshauriwa kuyatuma upya.

Kwenye tangazo lililochapishwa kwenye gazeti la Daily Nation, toleo la Oktoba 28, 2019, mchakato mpya utaanza katika kaunti za Baringo, Busia, Embu na Garissa na kukamilika Desemba 16 katika vituo mbalimbali kaunti za Kisumu, Murang’a, Kiambu na Tharaka Nithi.

Shughuli hiyo itaendeshwa katika ngazi ya kaunti ndogo.

Awali, shughuli hiyo ilipangiwa kuanzia Oktoba 27 lakini ikaahirishwa kufuatia malalamishi yaliyoibuliwa na wabunge kwamba vituo vya kuendesha shughuli hiyo havisambazwi kwa njia sawa.

“Jeshi la Ulinzi la Kenya lingependa kuwajulisha Wakenya kwamba shughuli ya usajili ambao awali uliahirishwa sasa imeritibiwa upya kuanza Novemba 27 hadi Desemba 16, 2019,” makao makuu ya KDF ikasema kwenye tangazo hilo.

Wale ambao walikuwa wametuma maombi awali, wameshauriwa kuwasilisha maombi yao upya. Hawa ni wale ambao wanataka kuajiriwa kama Kadeti, maafisa wa taaluma mbalimbali na mafundi ambao walituma maombi kwa makao makuu ya KDF.

Wale ambao wanataka kusajiliwa kama wanajeshi wa cheo cha konstebo ndio watahitajika kufika katika vituo vya usajili kuanzia Novemba 27 kufanyiwa usaili.

Wanaotaka kusajiliwa kama wanajeshi wa kawaida (servicemen) ni sharti wawe na umri wa kati ya miaka 18 na 26, wawe na urefu wa futi tano, wasiwe na rekodi yoyote ya uhalifu, wawe walipata angalau alama ya D+ katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE).

Vijana watakaoshiriki katika shughuli wameonywa dhidi ya kuwasilisha vyeti bandia vya masomo na kutotoa hongo yoyote kwa maafisa wanaoendesha shughuli hiyo.

“Wale ambao watajiwasilisha kwa usajili huo wakiwa na stakabadhi ghushi au wakipatikana wakishiriki shughuli za hongo watakamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria,” tangazo hilo likasema.

Likaongeza: “Hakuna malipo yoyote yanayotozwa wanaoshiriki usajili huo.”

Wabunge walipinga wazo la kuweka vituo vya usajili katika ngazi ya kaunti wakitaka shughuli hiyo igatuliwe hadi katika ngazi ya wadi.