Makala

USALAMA BARABARANI: Serikali kutumia Sh1bn kuimarisha sekta ya bodaboda

August 13th, 2019 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

KWA muda sasa, sekta ya bodaboda nchini Kenya imejipa taswira ya mauti ambapo hospitali zote kuu katika Kaunti angalau huwa zimetenga wadi za kushughulikia majeruhi wa ajali za pikipiki.

Kufikia mwaka wa 2030, mauti ya bodaboda yametazamiwa kuingia katika sababu tano ambazo huua Wakenya kwa ‘fujo’.

Vifo vinavyotokana na uchukuzi wa bodaboda kwa sasa vikipanda kwa kasi kubwa kutoka watu 35 mnamo 2007 hadi 268 mwaka 2018.

Aidha, mwaka 2018 watu 2,003 wamerekodiwa kwamba walipata majeraha ya viwango mbalimbali.

Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki husifiwa sana kuwa mwaka wa 2004 alileta mabadiliko ya sera katika ushuru wa pikipiki na ndipo vijana wengi ambao zamani wakihangaika, leo hii wameweza kukumbatia sekta hii kama ya kuwafaa kiriziki.

Hata hivyo, ni sekta ambayo kila uchao imekuwa katika vyombo vya habari kwa hili na lile zuri, lakini pia mabaya.

Baadhi ya wahudumu wa bodaboda wamemulikwa kuwapa wasichana wadogo mimba miongoni mwa uhalifu mwingine.

Kisa cha hivi karibuni kinahusu kuaga dunia kwa vijana wanane wa kiume wa kati ya umri wa miaka 19 na 24 ambao walifariki majuma mawili yaliyopita katika Kaunti za Kirinyaga na Nakuru.

Visa hivyo viwili vilihusisha pikipiki mbili, kila moja ikiwa ilikuwa imebeba abiria wanne.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Trafiki nchini, Luka Kimaru yapo matatizo mengi tu katika sekta ya uchukuzi wa pikipiki.

“Tuna shida kubwa hapa ya ulevi wa waendeshaji pikipiki, ukosefu wa utiifu kwa sheria za barabara na pia utundu wa kukataa kutii alama za barabarani ipasavyo,” akasema Bw Kimaru.

Kuepukika

Alisema kuwa mauti hayo yote ya wanane yangeepukika ikiwa katika hali zote, waliohusika walitii sheria za barabarani.

Sasa, kuzima jinamizi hili, serikali ikishirikiana na mashirika ya kibinafsi imetoa ruwaza ya thamani ya Sh1.5 bilioni kuifanya sekta ya bodaboda iwe salama kwa wateja ambao ni abiria na pia wahudumu.

Kwa mujibu wa afisa wa utekelezaji wa Ruwaza hiyo Bw David Mbithi Roberts, ajali zinazozua mauti ikihusisha bodaboda zimekadiriwa kuwa miongoni mwa sababu 10 za juu zinazosababisha mauti hapa nchini.

Bw Roberts anasema kwa sasa kuna bodaboda 91,898 ambazo zimesajiliwa katika sekta ya uchukuzi, hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 2000 kutoka mwaka wa 2005.

Ruwaza hiyo itatimizwa na kutathimiwa mwaka wa 2020, huku mikakati mingine ikiandaliwa ili kuijumuisha sekta hiyo kama lengo muhimu la Ruwaza ya 2030 kwa vijana.

Jacinta Syombua (aliyeketi nyuma) akiwa na bintiye Evelyn Mwendi (kati) katika pikipiki mjini Thika. Wawili hawa ni
vipofu na sekta hii ikiimarishwa bila shaka maisha ya abiria wengi na wahudumu wa bodaboda yatakuwa salama. Picha/ Mwangi Muiruri

Kufikia mwaka wa 2020, serikali inalenga kutoa elimu maalumu kwa maafisa wa trafiki 10,000 ili kuwahami na ujuzi wa kuthibiti sekta hii.

Kulingana na Bw Kimaru, mikakati hiyo tayari imezinduliwa ikilenga kuhamasisha waendeshaji bodaboda kuhusu wajibu wao wa usalama barabarani.

“Tushaanza kuwaelimisha wanabodaboda katika maeneo tofauti ya hapa nchini. Mwezi huu tutakuwa na elimu kwa wahudumu wa Kaunti ya Kiambu,” akasema.

Aidha, akaongeza, serikali kupitia kwa wafadhili itazindua silabasi ya vyuo vya kutoa mafunzo kwa waendeshaji pikipiki ambayo itaifanya kazi hiyo kuwa ya kitaaluma.

Juhudi hizi zitafanikishwa na kuundwa kwa kitengo cha kuhifadhi takwimu za maafa na pia majeraha na ufadhili uwekwe katika hospitali zote za umma kushughulikiwa wahasiriwa wa janga la ajali za bodaboda.

Kitengo hicho kitajulikana kama Injuries Prevention and Information Centre –Kenya (IPIC-K) na ambacho kitashirikiana na Wizara za Afya, Uchukuzi, Barabara, Usalama wa ndani, Vijana na pia Ustawi wa Vyama vya Ushirika.

Ruwaza hiyo inalenga kuifanya sekta ya bodaboda kuwa yenye kuunda nafasi za kazi kwa vijana wala sio mtindo wake wa sasa ambao unaunda maafa na majeraha kwa wateja na pia wahudumu.

Kwenye ruwaza hiyo, serikali inakiri kuwa sekta hii iliingia katika sekta ya Uchumi kwa ghafla na bila sera yoyote, hali ambayo imezua ugumu wa kuidhibiti.

“Kufikia sasa hali ya ajali za bodaboda imekuwa kero kubwa kwa hospitali za umma ambapo hatuna sera yoyote ya kushughulikia waathiriwa,” akasema Bw Roberts.

Ruwaza hiyo inataja uendeshaji pikipiki kwa kasi iliopindukia, elimu duni, utumiaji wa mihadarati na pia kutozingatia sheria na kanuni za barabara kama chanzo cha misiba katika sekta ya bodaboda.

Kwingineko, Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria tayari ametangaza mpango wa Sh1.14 bilioni wa kuwahami wanawake 1,000 wa eneo hilo na uwezo wa kushiriki riziki ya uchukuzi wa bodaboda.

Bw Kuria alisema kuwa bajeti hiyo itaundwa kwa msingi wa ushirika wa hazina ya maendeleo mashinani (NGCDF) na wahisani kutoka sekta ya kibinafsi.

Aliongeza kwamba walengwa wa mpango huo ni wale wanawake ambao hawana ujuzi wa kitaaluma, waliookolewa kutoka ulevi kiholela na wengine ambao wanaorodheka katika umaskini.

Alisema amesaka taasisi za kuendeleza masomo hayo ya uendeshaji bodaboda na ambapo kila mmoja atatozwa ada ya Sh14,000.

“Wakishapata huo ujuzi wa kuendesha pikipiki, nitawajumuisha katika mpango wa ushirika na ambapo tutasaka pesa zaidi za kuwapa uwezo wa kujinunulia pikipiki za uchukuzi,” akasema Kuria.

Alisema kuwa kwa sasa gharama ya kununua pikipiki moja ni Sh100,000 na ambapo ukijumuisha ile gharama ya kumhami mmoja wa wanawake hao na ujuzi wa kuiendesha, bajeti ya kila mmoja itakuwa Sh114,000.

Bw Kuria alisema kuwa hali ya umasikini mashinani inahitaji ubunifu ili kukabiliana nayo ikizingatiwa kwamba nafasi za ajira ni finyu na kuna changamoto ya wengi wa walio masikini na wako katika umri wa ujana kuwa hawana elimu ya kutosha ya kuwaingiza katika masomo ya kitaaluma.

Alisema kuwa kulenga kwake jumuia ya wanawake ni kutokana na hali halisi mashinani kuwa wanaume wengi ndio wako katika sekta ya bodaboda kwa kuwa wako na ule ujuzi wa kusukumana kimaisha hadi kuishia kuwa waendeshaji bodaboda.

“Sekta hii ni mojawapo ya zile ambazo zimeunda nafasi nyingi za kazi licha ya kuwa imeibuka pia kuwa hatari kwa afya ya umma kufuatia ajali za kiholela. Ajali hizo sanasana hutokana na aidha vijana hao kutokuwa na masomo rasmi kuhusu uendeshaji au kuingia kazini wakiwa walevi. Hali yangu ya kuwapenyeza wanawake katika sekta hii itakuwa na mikakati ya kuzima ajali hizo kupitia ujuzi wa kitaaluma na pia ule muungano wa ‘ushirika wa kumulika nidhamu‘,” akasema.

Kuria alisema anaamini akifanya hivyo na walengwa wajitume kuwajibikia uimarishaji wa mpango huo, basi umaskini Gatundu Kusini utapunguka kwa asilimia 30.

Alisema ataendelea kusaka fursa nyinginezo za kuwainua vijana wa eneo hilo, huku akiitaka serikali ya Kaunti ya Kiambu pia izindue mipango sambamba ya kuinua uwezo wa vijana wasio na ajira katika kaunti hiyo.