Habari Mseto

Usalama kuimarishwa msimu wa shamrashamra

October 23rd, 2019 1 min read

Na LAWRENCE  ONGARO

USALAMA utaimarishwa vilivyo msimu huu ambapo shamrashamra za Krismasi Desemba na Mwaka Mpya zinanukia, ili kulinda mali ya wananchi.

Naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Juja Bw Charles Mureithi, aliwajulisha wakazi wa Juja kwamba maafisa wa usalama kote nchini hawatakwenda likizo hadi Januari 2020.

“Mpango huo wa serikali uliafikiwa ili kuhakikisha mwananchi wa kawaida anaishi kwa amani na mali yake kulindwa,” alisema Bw Mureithi.

Akizungumza Jumanne katika shule ya msingi ya Mugutha, alisema wananchi wako huru kutoa habari zitakazosaidia serikali kuwanasa wahalifu.

Wakati wa mkutano huo afisa huyo aliandamana na kamanda mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Juja Bi Dorothy Migarusha, na afisa wa polisi OCS Juja Abel Mwarania.

Afisa huyo aliwahimiza wananchi popote walipo washirikiane kwa karibu na maafisa wa usalama ili kuhakikisha usalama unadumishwa.

“Kila mwananchi ana jukumu la kuona ya kwamba usalama unaimarika. Iwapo kutakuwa na ushirikiano huo, bila shaka kutakuwa na utulivu,” alisema Bw Mureithi.

Alilaumu watengenezaji pombe na wanaouza bangi kwa vijana.

Alisema tayari maafisa wa usalama wameanza kufanya msako mkali ili kukabiliana na kadhia hizo.

Alitoa mwito kwa viongozi wa makanisa wawe mstari wa mbele kuzungumzia maovu katika jamii.

“Ningetaka viongozi wa makanisa wajitokeze wazi ili kukosoa yale mabaya yanayotendeka katika jamii,” alifafanua.

Alisema uchunguzi uliofanya umabainisha ya kwamba bangi kiasi kikubwa siku hizo husafirishwa kutoka maeneo ya Magharibi na Nyanza hadi sehemu za Mlima Kenya.

“Tunaelewa vyema kuwa bangi hiyo tayari huwa imepata soko kwa watu fulani ambao kwa sasa wanasakwa na maafisa wa usalama,” alifafanua afisa huyo.

Alizidi kueleza kuwa vijana wengi wanastahili kupewa ushauri wa kiakili ili wafahamu ubaya wa kujihusisha na pombe na dawa za kulevya.