Usalama: Masomo yatatizika Baringo

Usalama: Masomo yatatizika Baringo

Na FLORAH KOECH

SHUGHULI za masomo zinaendelea kutatizika katika maeneo ya Kaunti ya Baringo yanayokabiliwa na mapigano mara kwa mara huku baadhi ya shule zikikosa kufunguliwa tangu 2005.

Shule 10 katika kaunti hiyo bado hazijafunguliwa kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, wazazi na watoto wao wakihama maeneo hayo ya vita wasirejee tena kwa kuhofia usalama wao. Wengi wao walihamia maeneo salama lakini watoto hawakurejea shuleni kuendelea na masomo yao.

Pia baadhi ya shule katika eneo hilo zinahitaji kukarabatiwa baada ya kuharibiwa vibaya na majangili waliojihami vikali huku ikiripotiwa mauaji ya watoto wa shule na walimu wakiuawa.

Kaunti ndogo ambazo ziliathiriwa vibaya na mapigano hayo ya mara kwa mara ni Baringo Kaskazini, Baringo Kusini, Baringo Kaskazini na Tiaty. Shule ambazo bado hazijafunguliwa tangu 2005 kutokana na ukosefu wa usalama ni Ramacha, Ruggus, Kamwetio, Chepkew, Loromoru, Barsuswo, Tandar, Katilomwo, Karkaron, Ng’elecha, Chepkesin na Chesitet.

Baadhi ya shule nazo zimekuwa zikifunguliwa kisha kufungwa tena baada ya mapigano kuchacha hali ambayo inavuruga sana ratiba ya masomo ya wanafunzi na walimu. Shule hizo ni Kapindasum, Kasiela, Sinoni, Arabal, Chemorong’ion, Mukutani, Noosukro,Yatya, Chemoe, Kesumet, Kagir, Loruk, Kosile, Barketiew na Kapturo.

Kwa mujibu wa wenyeji ukosefu huo wa usalama umechangia idadi ya chini ya wanafunzi kukumbatia masomo wengi wao wakiacha shule baada ya wazazi wao kuhamia maeneo salama ili kuyanusuru maisha yao.

Mzee wa kijiji cha Chemoe, Baringo Kaskazini Richard Chepchomei alisema kwamba ni vigumu kwa watoto waliotorokea usalama wao kujiunga na shule mpya jirani kwa kuwa ziko mbali na pia wanahofia watavamiwa tena katika shule hizo. Kwa hivyo, wengi wao huamua kuachana na shule.

“Ni jambo la kusikitisha kwa kuwa kuna maeneo ambapo jamii huenzi sana elimu kwa watoto wao lakini mara kwa mara shule hufungwa kutokana na uvamizi wa majangili. Watoto na wazazi wao hulazimika kuhamia maeneo mengine kwa sababu ya usalama wao; jambo linalokatiza masomo yao,” akasema Bw Chepchomei.

Katika baadhi ya shule za msingi ni wanafunzi wa gredi ya nne na darasa la nane ambao wanaruhusiwa kuendelea na masomo ili iwapo kunatokea uvamizi, basi ni rahisi kuwaondoa hadi maeneo salama.

Shule za msingi za Arabal na Kipindasim katika eneo hilo hukabiliwa na mapigano kwenye wadi ya Makutano, Baringo Kusini, ni wanafunzi wa kuanzia gredi ya nne hadi darasa la nane wanaoruhusiwa kufika shuleni.

Wanafunzi wa madarasa ya chini huwa wanasoma katika shule jirani za Chemorong’ion na Kasiela ambazo ni salama zaidi na watoto hao wadogo hawawezi kutembea kwa zaidi ya kilomita tano.

You can share this post!

UDA yaelekeza macho yake 2022 baada ya London

TAHARIRI: Serikali isubire ripoti kuhusu AstraZeneca