Habari

Usalama: Natembeya awataka Wakenya wayape masuala ya usalama zingatio kuu

July 20th, 2019 1 min read

KATE WANDERI na GEOFFREY ONDIEKI

WAKENYA wameshauriwa wawe waangalifu na kuchukulia masuala ya usalama kwa uzito ufaao, wakati huu ambapo ulimwengu unakumbwa na mashambulizi ya kigaidi.

Mshirikishi wa masuala ya serikali kuu eneo la Rift Valley, Bw George Natembeya, aliwataka wananchi wasipuuze jambo lolote dogo, linalohusiana na usalama wao.

“Tunaishi nyakati hatari ulimwenguni. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa chonjo wakati wowote, tujifunze kuwajua majirani zetu,” akasema Natembeya.

Bw Natembeya alieleza kuwa njia zote za kuwaingiza watu kwenye itikadi kali huanza mitaani, na hivyo wazazi wana jukumu la kuwafuatilia watoto wao wasinaswe kwenye mitego ya kujiunga na vikosi vya kigaidi.

“Wengi wa vijana wanaokubali kujiunga na makundi ya itikadi kali wanatoka katika jamii zetu. Wazazi wanafaa kuwa makini, hasa wakati vijana wanatoweka, wengi wakijiunga na makundi ya kigaidi. Vilevile, wazazi hawafai kutelekeza jukumu lao la kuwapa wanao mwongozo bora maishani,” akaongeza Bw Natembeya.

Vijana kusajiliwa na magaidi

Afisa huyo wa serikali aliwaomba washikadau wote kama serikali ya kitaifa na ile ya kaunti, wafanyabiashara na viongozi wa kijamii kushirikiana kwa lengo la kutokomeza mwenendo unaochipuka wa vijana kusajiliwa na makundi ya kigaidi.

Kaunti ya Nakuru Ijumaa ilikuwa ya kwanza kuzindua mpango na mikakati ya kupambana na ugaidi baada ya Rais Uhuru Kenyatta Juni 10, kuamrisha vita dhidi ya ugaidi vigatuliwe hadi kwa majimbo mbalimbali.

Rais aligiza kaunti zote kubuni njia ya kutokomeza dondasugu hilo alipofungua Kongamano la kukabiliana na ugaidi lililoandaliwa jijini Nairobi.