Habari Mseto

Usalama wa watoto ni muhimu kuliko ufunguzi wa shule – Wazazi

September 30th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Huku hali ya sintofahamu kuhusu ufunguzi wa shule hivi karibuni ikishuhudiwa, wazazi wameridhia kauli ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu usalama wa watoto.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alikuwa ametangaza kwamba shule zitafunguliwa Oktoba 19, 2020 nayo tume ya kuwaajiri walimu nchini, TSC ikiamuru walimu kurejea shuleni mnamo Jumatatu, Septemba 28, 2020 kwa maandalizi ya shughuli hiyo.

Kwenye hotuba yake kwa taifa, Jumatatu, Rais Kenyatta aliashiria huenda ufunguzi wa shule ukachelewa, kinyume na alivyotangaza Prof Magoha.

“Ninamhimiza Waziri wa Elimu tukikubaliana shule zitakavyofunguliwa, atoe kalenda ya masomo 2020 iwapo itawezekana au 2021. Hiyo italingana na hali itakavyokuwa na ikiwa tutakubaliana,” akasema Rais.

“Maisha ya watoto wetu na afya zao si suala la kuwekwa kwenye mjadala, shule zitafunguliwa wakati tutakuwa na imani na usalama wao,” akasisitiza.

Rais Kenyatta alitoa msimamo huo wakati akitangaza kulegeza baadhi ya sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti kuenea kwa Covid-19.

Kufungwa kwa shule zote nchini na taasisi za elimu ya juu, ni baadhi ya hatua zilizochukuliwa na serikali Kenya ilipothibitisha mkurupuko wa virusi vya corona Machi 2020.

Kufuatia kauli ya Rais Kenyatta kuhusu ufunguzi wa shule, baadhi ya wazazi wameiridhia wakisema serikali haijajiandaa kikamilifu kuhakikisha watoto wanazuiwa kuambukizwa corona shuleni.

“Shule nyingi za kibinafsi huenda zikashindwa kufungua kwa sababu ya ukosefu wa fedha kuafiki mahitaji, na ina maana kuwa idadi ya wanafunzi katika shule za umma itaongezeka kwa kiasi kikubwa. Shule za umma zimekuwa na upungufu wa madarasa, wengi wetu tutapeleka watoto humo na ni wazi itakuwa vigumu kuafikia kigezo cha umbali kati ya mtoto na mwenzake. Kimsingi, matamshi ya Rais yaliashiria kwamba serikali haijajiandaa kulinda watoto wetu,” Antony Kibue ameambia Taifa Leo.

Mzazi huyo wa watoto wawili anapendekeza ufunguzi uahirishwe hadi 2021, ikikumbukwa kuwa wataalamu wa afya wanaonya kuhusu mlipuko wa awamu ya pili wa maambukizi ya Covid-19 ikiwa uchumi utafunguliwa kikamilifu mara moja, huku kiwango cha maambukizi kikionekana kupungua.

Sawa na Bw Kibue, Michael Murimi anasema kulingana na athari za uchumi, ambapo wengi wamepoteza ajira kipindi hiki cha corona, hawana uwezo kurejesha watoto shuleni mwaka huu. “Wengi wetu tulipoteza ajira Covid-19 ilipoingia. Familia tumezipeleka mashambani na tunategemea vibarua vya hapa na pale, hatuna pesa kwa sasa kulipa karo,” Murimi akasema.

“Kipindi hiki mapato ni ya kukithi familia riziki. Tunahitaji muda tujipange kutafuta karo,” akasema Mary Lihasi, mama wa mtoto mmoja aliye katika kidato cha kwanza.

Mikakati iliyowekwa na serikali kuruhusu ufunguzi wa shule ni ghali kuafikia, na nyingi ya shule za kibinafsi zimetoa notisi ya kufunga kabisa shule zao.