Usalama: Wakuu wahakikishia raia

Usalama: Wakuu wahakikishia raia

Na KNA

KAMATI ya usalama katika Kaunti ya Mombasa, imehakikishia wakazi na wawekezaji kuwa kuna mipango ya kutosha ya ulinzi itakayohakikisha kuna usalama wakati wa uchaguzi.

Naibu Kamishna wa Kaunti, Bw Ronald Mwiwawi, alisema kamati hiyo inashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa kidini ili kuhakikisha amani na usalama zitadumishwa wakati wote wa uchaguzi na baadaye mjini humo.

“Uchaguzi ni shughuli ya siku moja ambayo haifai kamwe kuwa chanzo cha vita. Tumeweka mikakati ili kuhakikisha Mombasa kutakuwa na amani na utulivu,” akasema.

Alikuwa akizungumza baada ya kuhudhuria kongamano la Baraza la Maaskofu kuhusu kudumisha amani, ambalo lilileta pamoja viongozi wa makanisa mbalimbali.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Askofu Joseph Maisha, alikashifu wanasiasa ambao hutenganisha wananchi wakati wa kampeni, akaahidi kuwa viongozi wa kidini wamejitolea kuhubiri amani makanisani na kuhimiza waumini pia wafanye hivyo maeneo wanakoishi.

“Ninahofia kama tutashindwa kueneza habari za amani kwa sababu kuna watu wasiopokea habari hizi hasa walio katika maeneo ya mbali kutoka mijini. Kuna watu ambao ifikapo wakati wa uchaguzi, wao hutenganisha wananchi waliokuwa wakiishi kama ndugu na dada. Sisi tutahubiri ujumbe wa amani kwa waumini tukitumai watafikisha ujumbe huo mashinani,” akasema.

Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, Dkt Samuel Kobia ambaye ndiye alikuwa mgeni wa heshima katika kongamano hilo, alionya vijana ambao watakubali kutumiwakuzua vurugu wakati wa uchaguzi kuwa wataadhibiwa kisheria.

Dkt Kobia alisema maafisa wa NCIC wakati huu hawatafuatilia mienendo ya wanasiasa pekee bali pia wananchi watakaohusika katika kuchochea ghasia za uchaguzi.

“Tuna maafisa na vifaa vya kutosha ambao watanasa sauti na picha kutoka kwa mikutano ya kisiasa kwa hivyo tumejiandaa vilivyo,” akasema.

Aliongeza kuwa wamezindua hamasisho la kitaifa kwa lengo la kudumisha amani na umoja wakati wa kipindi cha uchaguzi.

Kulingana na Dkt Kobia, mashirika ya kidini yatakuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha uhamasishaji.

“Jamii za kidini ni muhimu sana katika juhudi za kupambana na ghasia za uchaguzi. Habari huwa zinaweza kuenezwa kutoka kwa wahubiri hadi kwa waumini ambao hutoka sehemu tofauti, na hivyo basi habari hizo zitafika mashinani,” akasema.

Alitoa wito kwa wadau wote wanaohusika katika maandalizi ya uchaguzi kuhakikisha kutakuwa na uchaguzi huru na wa haki bila ghasia ili kuwe na mandhari bora yatakayoendelea kuvutia wawekezaji wa kimataifa.

“Lengo letu ni kusaidia viongozi wa Kenya kubadilisha mienendo ambayo kila wakati wa uchaguzi huwa kuna wasiwasi miongoni mwa Wakenya,” akasema.

You can share this post!

Sonko awa mwiba kwa wanasiasa na maafisa serikalini

TAHARIRI: Ni usaliti kulipia mabwawa hewa Sh80b

T L