Makala

USANII: Kaunti ya Kitui yasaidia vijana kurekodi nyimbo

August 20th, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

SANAA – hasa uimbaji na uchoraji – imesaidia kubuni nafasi nyingi za ajira nchini.

Si tu katika sanaa za hizo, ila pia kughani mashairi, kujihusisha na michezo kama vile soka, riadha, magongo, judo, chesi, karate, gofu, hoki, voliboli, michezo ya kuigiza, mpira wa vikapu na miereka, hiyo ikiwa michezo michache tu kuorodhesha.

Vipaji wengi mitaani wamejaaliwa talanta za aina mbalimbali lakini hawajatambulika. Serikali ifahamu wazi kuwa wengi wanataabika na kuhangaika namna ya kuzipalilia.

Ukosefu wa fedha na hamasisho, ni miongoni mwa milima na mabonde wanayokwea angaa kukata kiu cha ndoto zao maishani.

Aidha, ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana haohao waliojaaliwa ni donda ndugu, ambalo limewazingira.

Kila mwaka, maelfu hufuzu vyuoni kwa vyeti mbalimbali vya elimu, asilimia kubwa wakiishia kukosa ajira.

Kijana Justus Nderitu maarufu kwa jina la lakabu kama Makaveli, ni muimbaji wa nyimbo za Hip-Hop.

Mwanamuziki huyu kutoka mtaani Mumbi, kaunti ya Kiambu, ametumia usanii wake kusifia wachoraji wa kurembesha magari.

Kwenye video ya kibao chake cha kwanza, ‘Bus Rider’, kinaonyesha na kusifu baadhi ya mabasi yanayohudumu jijini Nairobi yalivyopambwa nje na ndani kisasa kabisa.

Kwenye stanza kadhaa za wimbo huo, Nderitu anatambua michoro ya picha inayowapa promosheni wasanii wa humu nchini. Mkondo wake, ni wa kisasa, kidigitali, katika kuimba Hip-Hop.

“Tusipoinua sanaa na wasanii wetu, ni nani mwingine atakayechukua jukumu hilo? Ninahimiza kila mmoja, kuanzia serikali kuu, za kaunti, viongozi na mashirika yasiyo ya kiserikali tuungane kukuza vipaji wetu,” anaeleza Bw Nderitu.

Wimbo wa pili ni ‘Don’t You Cry’ unaotuliza nyoyo za waliokumbwa na taabu na mikasa tofauti.

Kibao cha tatu, ‘Ghetto Hero’ kinaangazia vipaji mitaani waliojaaliwa talanta mbalimbali, lakini hawana uwezo. Kinawapa motisha kwamba ipo siku shida zinazowazingira zitakuwa historia.

Nderitu alijitosa katika uwanja wa usanii 2015, na anasema safari haijakuwa rahisi.

“Hamasa na ukosefu wa fedha haswa kuingia studioni kurekodi ni baadhi tu ya changamoto nilizokumbana nazo. Pia, ni matatizo yanayofika wasanii chupukizi katika kila kona ya nchi,” anasema msanii huyu.

Alitambua amejaaliwa kipaji cha uimbaji 2011 akiwa shule ya upili.

Kitui, karibu kilomita 133, kutoka jijini Nairobi, tunakutana na Annastacia Mitau maarufu kama Prizzo Annastacia. Mwanadada huyu ni msanii wa nyimbo za injili kwa lugha ya Kikamba na Kiswahili.

Annastacia alitambua ana kipaji cha uimbaji akiwa katika shule ya msingi, miaka ya 2000.

“Nilikuwa nikitumba nyimbo kwa usaidizi wa maandiko ya Biblia. Niliwapa wanafunzi wenza kutumbuiza shuleni na hata kanisani,” anafichua muimbaji huyu.

Talanta yake katika uanamuziki aliendelea kuipalilia katika shule ya upili na taasisi ya elimu ya juu, ambapo amesomea ualimu.

“Katika shule ya upili nilishiriki mashindano ya nyimbo za Uswahilini kama vile Taarabu na Kaswida hadi kiwango cha kitaifa na kupokezwa vyeti,” Annastacia anasema.

Albamu yake ya kwanza ‘Mbiwie tei’ kwa Kiswahili ‘Nionee Huruma’ aliirekodi mwaka 2018.

Serikali ya Kaunti ya Kitui, kupitia Wizara ya Michezo, Vijana na Utamaduni, ndiyo ilimfadhili kurekodi vibao vyake.

“Nilitangulia kwa sauti (audio), na serikali ya Kaunti ya Kitui ndiyo iligharimia shughuli zote za studio,” anasema mwanamuziki huyu.

Mwaka huu, 2019, ameweza kunasa video kupitia ufadhili wa serikali ya kaunti ya Kitui chini ya uongozi wa gavana Charity Ngilu.

Annastacia aliambia Taifa Leo kwamba ilimchukua muda mrefu kuingia studioni kurekodi na hata kufanya video kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

Msanii huyu ni mwalimu wa shule ya msingi ya kibinafsi na ya bweni, St Gabriel, Mwingi na anasema amefanikiwa kubuni kilabu ya Muziki, Sanaa na Uigizaji shuleni humo.

Annastacia ndiye kiongozi wa kilabu hiyo na anaeleza kwamba anajivunia kunoa mwanafunzi mmoja wa darasa la nne, ambaye amejaaliwa kipaji cha uimbaji.

“Akimaliza kutunga albamu ya kwanza nitamsaidia kuingia studioni azirekodi,” anasema.

Albamu ya Annastacia Mitau, ‘Mbiwie tei’ ina nyimbo sita; Mbiwie tei, Ninakupenda Mungu na Neema, Niseng’ete – nimeshangaa, Lyikie vinya – jitie nguvu na Ninukilitye wasya – nimeinua sauti.

Bw Nephat Mbau ambaye amewahi kuhudumu kama produsa na fundi wa mitambo katika kituo kimoja cha redio nchini, ambapo alisaidia wananii kurekoidi nyimbo, anasema kizingiti kikuu kwa wasanii chipukizi ni ukosefu wa fedha.

“Kuna vipaji wengi katika ulingo wa muziki, lakini pesa hawana kugharamia shughuli za kurekodi vibao vyao na kunasa video. Serikali kupitia idara husika ichukulie suala hili kwa uzito,” anaeleza Mbau.

Pia, anahimiza wasanii chipukizi na mashirika yasiyo ya kiserikali wasaidie kuinua usanii na sanaa.

Vyombo vya habari, hasa redio na runinga, vinahimizwa kuwa katika mstari wa mbele kuinua wasanii chipukizi.

“Nyimbo za wasanii chipukizi ni vigumu kuingia kwenye vyombo vya habari, kwa sababu vinaegemea waliobobea,” anasema Annastacia Mitau, kauli inayoungwa na mwimbaji Justus Nderitu.

Hata hivyo, Bw Mbau anashauri haja ya kuzingatia utunzi bora wa nyimbo hasa sauti na produsa wanaoelewa vigezo vifaavyo.