Makala

Usanii ulivyomsaidia kukwepa makundi ya uhalifu Nakuru

February 24th, 2020 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Kuna njia mbalimbali ambazo mtu anaweza kujikimu kimaisha na akafanikiwa kiasi kikubwa, hii ndiyo sababu vijana wanahimizwa kufanya kazi yoyote bila kuchagua muradi iwe halali.

“Ingawa mwanzoni malipo hayawezi kuwa makubwa, ni bora kuliko kukaa bure.Aidha subira na ukakamavu ni mambo muhimu wakati binadamu anatafuta ufanisi,” anasema kijana Gilbert Emmanuel mhasisi wa kundi la vijana kutoka mtaani Langalanga kaunti ya Nakuru.

Gilbert anatumia sanaa ya kuandika, kuchora na kucheza ala za muziki ili kuwasaidia vijana wasiokuwa na ajira mitaani kujitenga na mihadarati , wapate jambo la kufanya.

Gilbert pia anawasaidia mabinti. Picha/ Richard Maosi

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali anasema alianzisha mradi huu mwaka wa 2009 mjini Nakuru, akiwa na lengo la kubadilisha dhana kuwa binadamu anaweza kujikimu kimaisha kupitia usanii.

Gilbert anashangaa kuona ni kwa nini vijana wengi wanasema hakuna ajira, ilhali kuna njia nyingi za kukidhi mahitaji ya kila siku mojawapo ikiwa ni kutumia vipawa vyao.

Kupitia mtandao wa kijamii Gilbert anaamini kuwa vijana wanaweza kupata jukwaa kubwa la kujitangaza na uungwaji mkono kutoka kwa mashabiki badala ya kutumia mitandao visivyo.

Makundi ya vijana wa jinsia ya kike na kiume yanatumika kuonyesha kuwa kupitia burudani kwa kuzingatia maadili mtu yeyote anaweza kujiajiri kwa kufikia kila rika.

“Kupitia sanaa ya kucheza ala za muziki nimefanikiwa kujiajiri na kuwaajiri wengine, jambo ambalo limenisaidia kujikwamua kimaisha kupitia raslimali kubwa ya ubunifu niliozaliwa nayo na kujifunza,”akasema.

Alieleza kuwa hata hivyo katika harakati ya kutafuta namna ya kujiajiri anaamini kuwa kuna baadhi ya vitu ambavyo mtu hawezi kufundishwa shuleni kabla ya kuanza kujitegemea.

Gilbert alieleza kuwa kwa sasa ana bendi yake ya zaidi ya vijana 100, kutoka Nakuru na miji mingine kama vile Eldoret na Nairobi ambapo wao hukutana angalau mara moja kila wiki kujipiga msasa.

“Baadhi ya mambo tunayozingatia ni pamoja na kulainisha sauti, kucheza ala za muziki, kuandika mashairi, kuigiza na kusakata densi, kila kundi likishughulikia jambo maalum,”akasema.

Anawahimiza vijana kutumia mazingira yao ili kupata mpenyo wa fursa nyingi zinazopatikana, atumie nafasi hiyo kuvuka mipaka na kutumia ubunifu wake kujipatia riziki.

Mwanzoni alitembea jijini Nairobi mnamo 2010 ndiposa akajifundisha kutengeneza muziki kisha akarejea Nakuru akilenga kuwasaidia vijana waliokuwa wamepoteza mwelekeo maishani.

Kulingana na Gilbert amejitwika jukumu la kuwasaidia vijana mtaani kujitafutia shughuli za kufanya akiamini kuwa vijana wengi wana talanta, isipokuwa hawana wahisani wa kuwashika mikono.

“Cha msingi ni kuhakikisha kuwa uwezo wa vijana haupotei bali unatumika kwa manufaa ya kubadilisha maisha yao kwa ajili ya kizazi cha kesho,”akasema.

Anasema alianza na tarakilishi moja bila sehemu maalum ya kujumuisha vijana wakati wa kufanya mazoezi kila siku za wiki.

Baadae alikodisha chumba karibu na eneo la Freehold ambapo angeweza kuhudumia idadi kubwa ya vijana kinyume na awali ambapo chumba chake finyu hakingeweza kuhimili idadi kubwa ya vijana.

Gilbert anasema kuwa kwa sasa amefanikiwa kuwasaidia vijana kutengeneza zaidi ya midundo 1000, na albamu ishirini ambpo amewasaidia vijana kufanya ushirikiano pia na wasanii waliobobea.

Gilbert anasema kazi yake ni kuwasaidia vijana kufikia upeo fulani katika taaluma yao ya muziki hatimaye, akawasaidia kutafuta soko la kuuza kazi zinazotokana na ubunifu wao.

Anasema kuwa harakati zake zimesaidia vijana wengi kupigana na janga la ukosefu wa ajira, changamoto kuu inayowakumba vijana siku hizi wengi wao wakionekana kukata tamaa na maisha.

Gilbert Emmanuel akiwa katika mtaa wa Langalanga kaunti ya Nakuru, akionyesha baadhi ya mitambo wanayotumia kutengeneza muziki. Picha/ Richard Maosi

Pamoja na hayo amekuwa akijumuika na vijana kwenye majukwaa mbalimbali kuwatumbuiza waumini wakati wa kesha,Koroga Festivals miongoni mwa tamasha nyinginezo nyingi zenye haiba kubwa nchini.

Mmoja wao aliyefaidika na mradi huu ni Nelly Hudson mwimbaji na mwigizaji ambaye anaimba nyimbo za kizazi kipya, amefanikiwa kutoa filamu mbili na kurekodi nyimbo mbili.

Nelly anasema kuwa kinyume na awali alikuwa akizungushwa kutoka kwenye studio moja hadi nyingine lakini sasa anaweza kujiandikia muziki wake na ukaweza kusikika kwenye vyomo vya habari..

Muziki wake umekuwa ukichezwa katika vituo vya redio na televisheni mjini Nakuru, jambo ambalo limemsaidia kupata mialiko arusini au kanisani kuwafurahisha watu wakati mwingine kwa malipo.

Hata hivyo anaomba vyombo vya habari kutoa fursa kwa vijana mashinani ili waweze kutangaza vipaji vyao kwa umma ili kuzima uhalifu katika mitaa ya mabanda.