Usasa ulivyoyeyusha utamaduni wa Ameru

Usasa ulivyoyeyusha utamaduni wa Ameru

NA WACHIRA ELISHAPAN

Jamii nyingi humu nchini zimekumbatia usasa wa mabara Amerika na Ulaya ambao kulingana na wazee wa jamii ya Ameru Njuri Ncheke utavikosesha vizazi vijavyo maana ya utamaduni.

Kulingana na Mzee Samson M’Ibiri (pichani juu), kinachochangia kuporomoka kwa mila na tamaduni ni utandawazi, ambao umebadili dunia ikawa uwanja mdogo wa kuchezea.

Wazee wengi nchini wamekosa umoja katika kuendeleza utamaduni huo wa kijamii kwa vijana ambao wako tayari kuupokea, jambo ambalo Bw M’Ibiri alikiri alipohojiwa na Taifa Leo Dijitali.

“Sisi kama wazee hatujakuwa na umoja, si mara moja tumekuwa tukivutana bila kufanya uamuzi wowote,” anasema.

Anadai kuwa kaida ambazo zilikuwa zikiongoza jamii sasa hazipo, si kwa sababu ya kukosa maana, bali kwa sababu zimetelekezwa .

“Kusema ukweli tumetelekeza majukumu yetu kama wazee. Hatujalivalia njuga suala hilo vizuri, sijui nani atatuokolea vijana wetu,” anaongezea.

Huenda jambo hili ndilo limechangia utepetevu wa maadili miongoni mwa vijana. Mzee M’Ibiri anasema kwamba katika jamii yao waliovunja ungo na kufikisha makamo ya kupashwa tohara walipaswa kufunzwa maadili na miongozo ya jamii hiyo kabla ya kupatana na kisu cha ngariba.

Baadhi ya matendo yanayodhihirishwa na baadhi ya vijana hayawiani na mafunzo ya unyagoni walikofunzwa namna ya kuishi na watu. Kulingana naye, mwngi yamesahaulika.

“Sisi tukiwa vijana tuliupenda utamaduni wetu. Sio kama leo hata vijana hawajali hawabali. Yasikitisha kuona jinsi ambavyo ujana wetu ulivyosahaulika. Mama na baba yangu walikuwa na jukumu la kulelea wana wao popote katika jamii yetu,” anasema.

Miongoni mwa yale anayopendekeza kuangaziwa upya,ni jinsi shughuli za kuziendesha shughuli za jandoni, akisema kwamba ndio msingi mkuu wa kufuata nyenzo za jamii.

Hata hivyo anawataka vijana kukubali kufunzwa mambo ya kijamii ili yawasaidie kabla ya kuegemea katika usasa ambao anasema bado hauhifadhi historia ya Afrika.

“Vijana nawaomba muwe tayari kufunzwa mambo yanayoendana na jamii zenu. Msiukumbatie usasa mkasahau mlipotoka, uafrika ndio rangi yako,” anarai mzee huyo.

 

 

You can share this post!

Kagwe akaangwa kuwatishia wahudumu wa afya

TAHARIRI: Mgomo wa maafisa wa afya utaleta maafa Krismasi