Habari Mseto

Ushahidi kuhusu aliyeuawa na kuzikwa mvunguni mwa kitanda wasakwa

December 18th, 2018 1 min read

ERICK MATARA na JOSEPH OPENDA

MAKACHERO mjini Nakuru Jumanne walikuwa wakijitahidi kupata ushahidi wa kutosha kuhusiana na tukio la uhayawani la mauaji ya mfanyavibarua mwenye umri wa miaka 55 ambaye mwili wake ulipatikana umezikwa chini ya kitanda chake.

Mwili wa Jared Sing’ori ulifukuliwa kutoka kaburi lenye kina kifupi chini ya kitanda chake katika kijiji cha Mzee Wanyama baada ya kutokomea kwa zaidi ya wiki moja. Mwili huo ulikuwa umeingizwa na kufungwa ndani ya gunia.

Mauaji hayo yameshangaza taifa na kuzua maswali kuhusu mtu aliyemuua na sababu haswa ya kumzika ndani ya nyumba yake tena chini ya kitanda.

Kulingana na Naibu Kamishina wa Nakuru Mashariki Herman Shambi, polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho na watafuatilia ushahidi muhimu utakaowaongoza hadi wamnase aliyemsafirisha marehemu ulimwengu wa ahera.

“Makachero wanaendelea kukusanya ushahidi muhimu na pia wanamsaka kijana aliyekuwa anaishi na marehemu. Barobaro huyo hajaonekana tangu marehemu apotee machoni pa umma,” akasema Bw Shambi.

Majirani hata hivyo walisema kwamba, marehemu alitokomea kwa zaidi ya wiki moja na kuwapa wasiwasi kuhusu alikokuwa na iwapo alikuwa salama.

Hata hivyo swali hilo lilijibiwa Jumatatu jioni wakati waliamua kulivalia njuga suala hilo kwa kuvunja nyumba ya mwendazake ndipo wakapata alikuwa amezikwa kwenye kaburi chini ya kitanda chake.