Habari Mseto

Ushahidi wa chuo cha Kampala kumtetea gavana wa Wajir watupwa

November 22nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Wajir Abdi Mohamud Alhamisi alipata pigo Mahakama ya Juu ilipotupilia ushahidi kutoka Chuo Kikuu cha Kampala International kuthibitisha alihitimu na shahada.

Ushahidi uliokataliwa ulikuwa wa naibu wa Chanzala Badru Dungu Katerega na msajili Bw Hamza Segawa.

Jaji Mkuu (CJ) David Maraga, Majaji Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang , Njoki Ndung’u , Smokin Wanjala na Isaack Lenaola waliukataa ushahidi huo wa wasomi hao wakisema “ulicheleweshwa mno kuwasilishwa mahakamani.”

Ushahidi ulikuwa ni afidaviti za Mabw Katerega na Segawa. Wawili hao walikuwa wamesema kuwa Bw Abdi alikuwa mwanafunzi chuoni humo kati yam waka wa 2009 na 2012.

Mwezi uliopita Bw Mohamud alikana madai hakuwa amehitimu kwa shahada ya digirii.

Wizara ya mashauri ya ndani ya Uganda ilikuwa imesema Gavana huyo hakutembelea nchi hiyo katika kipindi hicho anachodai alikuwa chuoni kati ya 2009 na 2012.

“Tumethibitisha kuwa hakuna rekodi yoyote inayothibitisha Bw Mohamud aliingia nchini Uganda kati ya 2009-2012,” alisema Bi Lynette Bridget Boganza katika barua aliyoandikia Mahakama mnamo Oktoba 22 mwaka huu.

Ushindi wa gavana huyo alibatilishwa na Jaji Alfred Mabeya kwasababu hajahitimu na shahada ya digirii.

Ni sharti kila Gavana awe amehitimu kwa shahada ya digirii ndipo afaulu kuwania kiti hicho.

Mahakama ya rufaa ilikubaliana na Jaji Mabeya kuwa Bw Mohamud hakufaulu kuwania kiti  hicho cha Ugavana kwa kukosa shahada ya digirii.

Wakimkubalia Bw Mohamud kuwasilisha ushahidi CJ Maraga , majaji Ibrahim, Ojwang’, Wanjala, Njoki na Lenaola walisema gavana huyo hakupewa fursa ya kuwasilisha ushahidi wote.

Akimtimua kazini , Jaji Mabeya alisema Bw Mohamud hakufaulu kuteuliwa.