Ushahidi wa kesi za ufisadi ni dhabiti – Rais

Ushahidi wa kesi za ufisadi ni dhabiti – Rais

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta ameelezea matumaini yake kwamba washtakiwa wa ufisadi watapatikana na hatia na mali za umma zilizofujwa zitarudishwa mikononi mwa wananchi.

Akizungumza akiwa Paris, Ufaransa ambako alihudhuria kongamano la kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, Rais Kenyatta alisema kuwa anaamini ushahidi uliowasilishwa kortini kuhusiana na kesi hizo unatosha kuthibitisha ufisadi ulitendeka na hivyo basi kazi sasa iko mikononi mwa idara ya mahakama.

“Tunaamini tuna kesi thabiti na tulifanya uchunguzi wa kina ilivyohitajika. Sasa tunasubiri kuona kile ambacho mahakama itafanya. Nina imani kwamba mahakama itatenda haki kwa Wakenya,” akasema, katika mahojiano na kituo cha televisheni cha habari cha France24.

Kesi za ufisadi wa mabilioni ya pesa za umma dhidi ya maafisa wakuu serikalini na wandani wao ni mojawapo ya masuala ambayo Rais anatazamia zitamwezesha kuacha sifa bora atakapoondoka mamlakani wakati kipindi chake cha pili cha uongozi kitakapokamilika mwaka wa 2022.

Jubilee

Ingawa ufisadi uliharibu sifa ya Serikali ya Jubilee hasa katika kipindi cha kwanza cha uongozi kilichoanza mwaka wa 2013, mabadiliko ya uongozi katika Idara ya Upelelezi wa Jinai na Idara ya Mashtaka ya Umma yalifanya mamia ya washukiwa kukamatwa na kushtakiwa kwa madai ya kufuja pesa za umma katika Serikali Kuu na za Kaunti.

Miongoni mwa mashirika ya umma ambayo yaliathiriwa ni Huduma za Vijana kwa Taifa (NYS), Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), Shirika la Usambazaji Umeme nchini la Kenya Power na Kampuni ya Mafuta nchini ya Kenya Pipeline.

Visa vingi vya ufujaji vilitokea katika ulipiaji wa huduma na bidhaa katika mashirika hayo ambapo imesemekana maafisa walipandisha bei kupita kiasi ili kujinufaisha pamoja na washirika wao.

Baadhi ya wakosoaji wa serikali wamekuwa wakitilia shaka iwapo kukamatwa kwa washukiwa wengi kutazaa matunda katika vita dhidi ya ufisadi kwani kesi nyingi za awali kama vile sakata katika Wizara ya Afya na ya kwanza ya NYS hazijawahi kukamilishwa.

You can share this post!

Kitendawili kuhusu michoro ya graffiti kwenye matatu kama...

SHERIA BARABARANI: Hatia za trafiki zitakazowatupa seli...

adminleo