Habari Mseto

Ushahidi wa Uhuru na Raila hautakikani, mahakama yaamuru

November 10th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

JITIHADA za walinzi wawili katika hoteli ya kifahari ya New Stanley za kutaka wapewe taarifa za ushahidi za Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga katika kesi inayowakabili ya kusambaza kinyume cha sheria katika mitandao video ya wawili hao wakitembea katika barabara ya Kenyatta Avenue, Nairobi usiku kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ilitipuliwa mbal na mahakama.

Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Nairobi Bw Bernard Ochoi alisema taarifa za ushahidi za Rais Kenyatta na Bw Odinga hazihitajiki katika kesi hiyo.

Bw Ochoi alisema ombi la Patrick Randing Ambogo na Janet Magoma kupitia kwa mawakili wao Danstan Omari na Apollo Mboya halina mashiko kisheria.

Randing na Janet wanakabiliwa na shtaka la kunasa kanda ya kamera za CCTV zilizoko katika hoteli ya New Stanley ya Rais Kenyatta na Bw Odinga wakitembea katika barabara ya Kenyatta usiku wa Juni 2 2020.

Wawili hao walinaswa wakitembea kwa miguu kwenye kinjia kilichotengenezwa na mamlaka ya kusimamia huduma za jiji NMS chini ya usimamizi wa Meja Jenerali Mohamed Badi.

Bw Ochoi alisema haoni umuhimu wa taarifa za ushahidi wa Rais Kenyatta na Bw Odinga katika kesi dhidi ya wawili hao.

“Nimefikia uaamuzi kuwa ombi hili la wawili hawa halina mashiko kisheria na la kiupuzi,” Bw Ochoi alisema.

Washtakiwa wanadaiwa walisambaza video hiyo katika mitandao ya kijamii ya Rais na Odinga wakigagua barabara mwendo wa saa mbili na dakika 20 usiku wa Juni 2 2020.

Wawili hao wanashtakiwa kwa kudugua kanda hiyo ya CCTZ kinyume cha sheria nambari 179 za uhalifu wa kimitandao.

Baada ya kushtakiwa wawili hao waliomba korti iamuru wapewe nakala za taarifa za ushahidi wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ambao usalama wao ulidaiwa ulitishwa.

Upande wa mashtaka umesema kuwa hautazamii kuwaita Rais Kenyatta na Bw Odinga kuwa mashahidi katik kesi hiyo.

Mawakili Omari na Mboya walieleza mahakama kuwa ushahidi wa walalamishi hao wawili (Kenyatta na Odinga) ni muhimu kisha wahojiwe.

Pia walikuwa wameomba wapewe nakala ya kanda hiyo.

Katika uamuzi wake Bw Ochoi alisema ni juu ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuchagua wataofika kortini kama mashahidi.

Washtakiwa wako nje kwa dhamana ya Sh10,000 pesa tasilimu.