Mashairi

Ushairi wa Jumamosi: ‘Mswada Sumu’

June 22nd, 2024 4 min read

Wabunge waheshimiwa, natuma ombi kufika,
Gazetini kuwekewa, Taifa Leo tajika,
Na mantiki limetiwa, kote Kenya kusomeka,
Rekebisheni mswada, wa kifedha una sumu!

Ujumbe mshaupewa, wetu bungeni peleka,
Hatukubali elewa, mswada ni wa dhihaka,
Damu twaja kamuliwa, na tayari kakauka,
Rekebisheni mswada, wa kifedha una sumu!

Vije kulazimishiwa, kitu tusichokita,
Eti ndicho chatakiwa, kwa nchi kuimarika,
Yakini tumezidiwa, kuteleza kuanguka,
Rekebisheni mswada, wa kifedha una sumu!

Hamwoni tunauliwa, nani aje kutuzika,
Bei tukipandishiwa, bidhaa anavyotaka,
Nini kitanunuliwa, uchumi utaanguka,
Rekebisheni mswada, wa kifedha una sumu!

Hapa mnashauriwa, tafadhali wheshimika,
Kilio kuzingatiwa, kote kinachosikika,
Mkwepe kulaaniwa, umma ujapodhurika,
Rekebisheni mswada, wa kifedha una sumu!

Nyie mlichaguliwa, msifanywe vibaraka,
Mihuri ya kutumiwa, na mtu anavyotaka,
Hatakubali Moliwa, si lema mkikumbuka,
Rekebisheni mswada, wa kifedha una sumu!

Busara inatakiwa, kila leo kutumika,

Kwa ndani kuangaliwa, kuna kupanda kushuka,
Leo mu waheshimiwa, hino kesho mwaondoka,
Rekebisheni mswada, wa kifedha una sumu!

Wino nimekaukiwa, ni mengi ya kuandika,
Hassan hapo ukiwa, ninakushukuru kaka,
Kwamba muda nimepewa, gazetini kusikika
Rekebisheni mswada, wa kifedha una sumu!

NYAGEMI NYAMWARO MABUKAH
“MALENGA WA MIGOMBANI”
MIGOMBA YA ZIWA KUU

Elimu ni muhimu

Shairi ninaanzia, kwa hivyo makinikeni,
Leo nawaelezea, nawasihi tulieni,
Nasema hutajutia, unapofunzwa shuleni,
Elimu nawaambia, ni muhimu duniani,

Elimu husaidia, Nyeri hadi Mombasani,
Masomo huendelea, Kenya hadi Marekani,
Kila mtu anafaa, kusoma hadi mwishoni,
Elimu nawaambia, ni muhimu maishani.

Ruiya ikitimia, ni bidii ninasema,
Walimu wanapitia, shuleni na ni lazima,
Hawa wahandisi pia, ni kupitia kusoma,
Elimu nawaambia, ni daraja ya maisha.

Daktari hutumia, elimu ‘sipitalini,
Barua tukiendea, tunampata Karani,
Kesi tunapotatua, wakili twahitajini,
Elimu nawaambia, inatupa maarifa.

Tamati nimefikia, kalamu chini naweka,
Sitaki mkijutia, vyema nimeeleweka,
Msije mkashangaa, nikienda Amerika,
Ni elimu nawambia, itanifikisha huko.

DEAN MUTUGI
MWANAFUNZI WA SHULE YA DAWN VISION.
MWEA- KIRINYAGA

Avieta

Ni zimwi limetufika, kwa vijana na wazee,
Duniani limezuka,yabidi tulikemee,
Kwa mapanga na mashoka, liende litokomee,
Mchezo huu wa ndege,ni tikiti ya mauti.

Wengine watajirika, kutokana na mchezo,
Wao huwa watosheka, wakifyata maagizo,
Wale wakudanganyika, huishia Kwa mabezo,
Mchezo huu wa ndege, ni tikiti ya mauti.

Watia Kwa kutetemeka, uwekapo hizo hela,
Ndege inapotoweka, wakosa hata kukula,
Bakunja na wakuteka, wabakia kuwa fala,
Mchezo huu wa ndege, ni tikiti ya mauti.

Wakopa bila mipaka, vijisenti vya kucheza,
Ukishindwa wateseka, unaishi Kwa kuwaza,

Ukata unakushika, washindwa kujiongoza,
Mchezo huu wa ndege, ni tikiti ya mauti.

Vita kufa kuponyeka, mchezo wa avieta,
Unayaleta mashaka, balaa nayo matata,
Ni laana na baraka, baraka wanaopata,
Mchezo huu wa ndege, ni tikiti ya mauti.

Ukianza hutatoka,unazo za kishetani,
Huwezi na kuepuka,wakuketisha na chini,
Macho zungukazunguka,na vidole kiwamboni,
Mchezo huu wa ndege, ni tikiti ya mauti.

Ujue ulikotoka, ulinde wako uzima,
Wacha hizo hekaheka, huyafanye yale mema,
Bure tu utafyatuka, ulie bila kukoma,
Mchezo huu wa ndege, ni tikiti ya mauti.

ANN MWANÀSARIFU
MWANANAKSHI SIMBAJIKE
VILIMANI KISII

Madhila

Kwenda mbele sikuwezi, balaa kurudi nyuma,
Nani wangu mtetezi, aje japo kwa rukwama,
Langu pambo sisimizi, mwilini wananiuma,
Madhila haya madhila, watu wanakosa utu.

Simi wa embe mkwezi, nilipo mi nalalama,
Nipo kwenye utelezi, taukweaje mlima,
Nimeubakiza uzi, kudondoka si gharama,
Madhila haya madhila, watu wanakosa utu.

Pendo lako wazi wazi, mama ulimpa jema,
Ukamwita laazizi, damu kwako asukuma,
Baba ukawa pwaguzi, hukurudi tena nyuma,
Madhila haya madhila, watu wanakosa utu.

Hayupo baba mzazi, katelekeza kwa mama,
Hajakubali malezi, aendekeza hujuma,
Nionekane mwenyezi, imara nijesimama,
Madhila haya madhila, watu wanakosa utu.

Twatiwa kwa vifukizi, tushindwe hata kuhema,
Haikomi michirizi, nayo sauti kukwama,
Vyazingira vizuizi, mama iwapi huruma,
Madhila haya madhila, watu wanakosa utu.

Nalia kwa mahimizi, kihimiza hima hima,
Haujautaka uzazi, wacha ngono za kinyama,
Subira isiwe kazi, kisha haina lawama,
Madhila haya madhila, watu wanakosa utu.

Beti nane siongezi, kuwachosha wanadama,
Lana mimi siliwazi, hapa ninadema dema,
Langu kwenu ni pongezi, muhukumu ni karima,
Madhila haya madhila, watu wanakosa utu.

NYAA EDISON
JICHO LA KUKU
RABAI, KILIFI

Mvulana hajaliwi!

Idhini Edita nomba, nilonge yalo ndaningu,
Ni kero ilonikumba, nilengapo ni uchungu,
Ninalemewa kuamba, ni kilio wanguwangu,
Lo! Mwana awe kiume, nyi mwamini hajaliwi!

Ni kihoro menitamba, meatuka moyoningu,
Matatizo meyasomba, haki zetu ni ukungu,
Mahangaiko twaramba, alijuaye ni Mungu!
Lo! Mwana awe kiume, nyi mwamini hajaliwi!

Wazazi wanatugomba, kutuzaba kali rungu,
Walimu nao ja simba, wakitufunza kizungu,
Hawatwelewi wajomba, kijidai kuwa jungu,
Lo! Mwana awe kiume, mwaminini hajaliwi!

Vichwa vyetu vimevimba, hatujatulia tangu,
Hatuna la kujigamba, adha metanda ja wingu,
Twakosa wa kutupamba, ila tumetiwa pingu!
Lo! Mwana awe kiume, nyi mwamini hajaliwi!

Gange nzito kama mimba, zi aushini muangu,
Kwamuka kila liamba, kwipiga deki mivungu,
Kukosa nyama magamba, pia kuhiniwa dengu,
Lo! Mwana awe kiume, nyi mwamini hajaliwi!

Kyume apewa kasumba, kuathiri wake wengu,
Raha kusakata rumba, kwa sauti kama gungu,
Kuonewa wani namba, kwa kiume si uungu!
Lo! Mwana awe kiume, nyi mwamini hajaliwi!

Ewe Mungu Mtuumba, ulete baraka kwangu,
Wanijali kuniremba, e babangu na mamangu,
Wasinitenge ja kimba, nishangilie kwishingu,
Lo! Mwana awe kiume, nyi mwamini hajaliwi!

Watamati la kulumba, situngi tena mafungu,
Nisifikishwe kizimba, kufichuangu machungu,
Mwana kiume kuyumba, tumalizeni wezangu,
Lo! Mwana awe kiume, nyi mwamini hajaliwi!

JAMES MUTWIRI WANJAGI,
“MALENGA MSIFIKA NA MSIKIVU”
CHUKA – THARAKA NITHI.

Ipo siku ya mawio

Matuta nazo kokoto, vimetamalaki njia,
Kulia nako kushoto, siwezi kuingilia,
Tanuri na mitokoto, Mirumbe yanizidia,
Ipo siku ya mawio, Mola ataniruzuku.

Imekwida moyo ndoto, natamani kutimia,
Tangu enzi za utoto, hakika imekamia,
Japo tele ni fukuto, maisha zimevuvia,
Ipo siku ya mawio, Mola ataniruzuku.

Situmii misokoto, ukweli huno sikia,
Nimepata michonyoto, ajira nikisakia,
Maneno ya mikongoto, donda yameniachia,
Ipo siku ya mawio, Mola ataniruzuku.

Si sekondari kidato, wa chuo asili mia,
Sijapata katu wito, maofisi nabishia,
Amini napunga joto, bila kazi asilia,
Ipo siku ya mawio, Mola ataniruzuku.

Sina sinani mpoto, hafifu nakiakia,
Zisiwadanganye foto, ningali sufuri gia,
Moyoni nanga nzito, mema nikitarajia,
Ipo siku ya mawio, Mola ataniruzuku.

Bahari maziwa mito, ng’ambo nitaifikia,
Nchi kavu miburuto, haki nitavumilia
Tamausho na masuto, haitabadili nia,
Ipo siku ya mawio, Mola ataniruzuku.

Baraka ya manyonyoto, ewe Mola nyunyizia,
Niandike tungo moto, kila mja kusifia,
Maneno pamwe mvuto, riwaya tamthilia,
Ipo siku ya mawio, Mola ataniruzuku.

Sina njia ya mkato, Mola natumainia,
Ayaondoe mapeto, ya sura kuharibia,
Nisipate mchecheto, wa kiwewe kunitia,
Ipo siku ya mawio, Mola ataniruzuku.

MIRUMBE NICKSON PETER
“USTADHI BABU KIJANA”

Natamani niko nawe!

Yalivyo mapenzi yako,mpenzi wangu Farida,
Kushinda moto wa jiko,kila kukicha ziada,
Kokote kule nendako,hata simalizi muda
Natamani niko nawe!

Sijui ulinipani,mwilini kikaenea,
“nakupenda si utani”hilo nalirejelea,
Kwako sioni lakini,usichoke endelea!
Mpenzi wanijulia!

Wajua nipewe vipi,kiasi hata vipimo,
Sikondi na sinenepi,katikati nimo humo,
Nakuwazia u wapi?Nauhisi mzizimo,
Jua nayafurahia!

Tangu kuche nina hamu,niseme nawe hakika,
Si kusema kwenye simu,ingawa nitasikika,
Lengo tupate taimu,tuseme huku twacheka!
Hamu ipate nondoka!

Ijapo ni wengi wake,walojazana mjini,
Wana umbile la kike,ujue nimebaini,
Ninasema nisikike,kama kwamba siwaoni,
Nilomuona ni wewe!

MOHAMMED .S. ALI
BABAYE AHMAD
KONGOWEA KWA KARAMA