Mashairi

USHAIRI WENU: Mtima wangu tulia

April 27th, 2019 4 min read

Mtima wangu tulia

Mtima wangu sikia, jifunze kuvumilia,
Mtima wangu tulia, machungu yapokujia,
Mtima wangu umia, lakini usijelia,
Mtima wangu tulia, jifunze kuvumilia.

Mtima wangu sikiza, koma kuniaibisha,
Komata kuutangaza, udhaifu wa maisha,
Mwili wangu kuuguza, maumivu yanachusha,
Mtima wangu tulia, jifunze kuvumilia.

Mtima wangu hakika, umeniponza yakini,
Ukiitwa waitika, yeyote wamuamini,
Ukipendwa wapendeka, bila ya kuwa makini,
Mtima wangu tulia, jifunze kuvumilia.

Mtima wangu kwanini, usiwe kama wa mama,
Mtimake natamani, ulivyoshinda dhuluma,
Umempa tumaini, hata we hebu tazama,
Mtima wangu tulia, jifunze kuvumilia.

GILBERT KINARA
Keumbu, Kisii

 

Wacha mahaba ya kifafa

Wangwana naungulika, nijuzeni nibaini,
Akili yavurugika, nipembejeni wendani,
Nti hini patashika, imejawa hayawani,
Penzi la kata na shoka, maana yake ni ipi?

Mpenzi si oksijeni, akikuwata utafa,
Wata kuwa limbukeni, wa mahaba ya kifafa,
Sikufiti ni uhuni, kusababisha maafa,
Penzi la kata na shoka, ndilo penzi la kisasa?

Penzi hutaka ujuzi, usidhani wazo pesa,
Kudekeza si upuzi, huba hutaka msasa,
Maina mi si mjuzi, wacho kisa na mikasa,
Penzi la kata na shoka, hatima yake ni ipi?

FRANCIS MAINA MACHARIA
‘Bin Macharia’
Kisauni, Mombasa

 

Yamerudi malumbano

Faida ya malumbano, kulumbana gazetini,
Hupata yalo manono, kukufaa akilini,
Yahadithiwa vigano, na misemo ya zamani,
Yarudiwa malumbano, ya watungaji mabingwa.

Kunayo mengi mavuno, ya watunzi wa zamani,
Kina Shamte mfano, mtunzi mwenye thamani,
Mimi humpenda mno, kwa yake mengi makini,
Yarudiwa malumbano, ya watungaji mabingwa.

Tuwaombea malenga, zamani waliotunga,
Waliojua kunga, mashairi kuyapanga,
Mola uwape muanga, na peponi kuwapanga,
Yarudiwa malumbano, ya watungaji mabingwa.

Malumbano tuapenda, twaburudi wasikizaji,
Fikira njema twaunda, ambazo zatufariji,
Na mili yetu yawanda, huku kuliko vijiji,
Yarudiwa malumbano, ya watungaji mabingwa.

MOHAMED YUSUF
Kisauni, Mombasa

 

Achana na sponsa

Vipusa wote nchini, yafaa kujiheshimu,
Mwajitia taabani, sasa tunawashutumu,
Fulusi ni akilini, mwazitafuta kwa hamu,
Sponsa wanawamaliza, pesa sio kila kitu.

Masomo zingatieni, ni maana kwa maisha,
Tabia za ughaibuni, mkiiga mtaisha,
Toa nta sikioni, ninataka kuwapasha,
Sponsa wanawamaliza, pesa sio kila kitu.

Sasa mwaitwa kunguni, hamuoni ni aibu,
Mwafikiri ni utani, hamna hata adabu,
Mwishowe ni kaburini, pasipo nayo kutubu,
Sasa wanawamaliza, pesa sio kila kitu.

Mjikubali vyuoni, msikuwe na tamaa,
Msilale shambironi, sponsa wanawatumia,
Aila zao nyumbani, wabaki wakiwalia,
Sponsa wanawamaliza, pesa sio kila kitu.

LIONEL ASENA VIDONYI
‘Malenga Kitongojini’
Seeds High School, Kitale


Nifanye nini?

Zao hili Simbaume, lanizolea mafuu,
Naomba leo niseme, moyo upate nafuu,
Swali kwenu nilitume, twambizane kama nduu,
Huyu mwizi nanukuu, nifanye nini akome.

Nalikesha gumegume, shambani kibahauu,
Nikisubiri achume, miraa sio tambuu,
Nimrukie kwa sime, nimkomeshe bunguu,
Huyu mwizi nanukuu, nifanye nini akome.

Jibu hili mlitume, linitoke hili buu,
Nimpe sumu akome, au chambo jungu kuu,
Kilishika hili ndume, hadi kwa chifu mkuu,
Huyu mwizi nanukuu, nifanye nini akome.

Beti nne nituame, hapo nalikata guu,
Swala hili mlipime, mnijuze maafuu,
Washairi mlitume, usipite mwaka huu,
Huyu mwizi nanukuu, nifanye nini akome.

MAINAH ALFRED MAINAH
‘Msanifu Makamula’
Mia Moja, Timau

 

Mtoto nadhulumiwa

Inakuaje jamani, wengine wenu hakika,
Binadamu duniani, umero umewafika,
Aliyewatuma nani, kuchafua Afrika,
Mimi mtoto wa kike, nazidi kudhulumiwa.

Aliyewatuma nani, kututendea unyama,
Hamtaki masomoni, tuwe sisi wa kusema,
Haipiti na jioni, visa vingi vyaandama,
Mimi mtoto wa kike, nazidi kudhulumiwa.

Haipiti na jioni, wenyewe mnatambuwa,
Kukeketwa hadharani, uchungu lazimishiwa,
Baadaye harusini, wachanga twaandaliwa,
Mimi mtoto wa kike, nazidi kudhulumiwa.

Baadaye harusini, dume lishachaguliwa,
Mimba kujibebeani, hakuna wakuambiwa,
Ndoto zangu kuzimuni, vipaji kukatiziwa,
Mimi mtoto wa kike, nazidi kudhulumiwa.

MUKOYA AYWAH
‘Malenga Mpelelezi’
Lang’ata, Nairobi

 

Mtoto ni yule wako

Mtoto hazai wako, ulomzaa mwenyewe,
Asiye wa ndugu yako, huyo usitegemee,
Awe hasa damu yako, uliyemzaa wewe,
Mtoto ni yule wako, ulomzaa mwenyewe.

Hata awe na vituko, ikiwa ni wako wewe,
Moja siku jua iko, yaja umtegemee,
Lakini wa ndugu yako, si wako hilo ujue,
Mtoto ni yule wako, uliyezaa mwenyewe.

Mtoto wa ndugu yako, siye wako ulijue,
Huyo ni wa ndugu yako, nawe wako jizalie,
Asikupe hangaiko, na tabu ujizuzue,
Mtoto ni yule wako, ulimzaa mwenyewe.

Nimeshaona vituko, sababu nielezee,
Na mengi mahangaiko, wa ndugu apendezewe,
Mwisho kanipa sumbuko, sababu nielezee,
Mtoto ni yule wako, uliyezaa mwenyewe.

SIWAJUMBE AMADI
Ngamiani, Tanga Tanzania


Tuthamini maisha

Tuzindukeni njozini, nawarai kishairi,
Tuzinduke walalani, hamaniko kishamiri,
Tuone tuilaani, kwa lazima kikahiri,
Tuzindukeni tayari, kukabili ukatili.

Tuzinduke kihisia, tuwe na utu wandani,
Tuweze kuhurumia, na maisha kuthamini,
Chonde kokote dunia, haki zetu tupateni,
Tuzindukeni tayari, kukabili ukatili.

Tuzinduke tusilale, gizani tukosekane,
Tukose na mizingile, Afrika tupendane,
Tuweze ishi na wale, wenye kero sikosane,
Tuzindukeni tayari, kukabili ukatili.

Ni hayo tu nasifia, Mjali siha kitua,
Tughairi mbaya nia, sithubutu kubagua,
Tuzidi kutamania, kuishi pasi kuua,
Tuzindukeni tayari, kukabili ukatili.

TONEY FRANCIS ONDELO
‘Malenga Mjali Siha’
Ndhiwa

 

Utangamano dawa

Naamba tega sikiyo, na pia uwe makini,
Mekisikia kiliyo, kilo kite nyingi yani,
Basi maji niyanywayo, nasafisha niwambeni,
Sote tukitangamana, tamaliza donda dugu.

Hili donda la uchoyo, halina wema yakini,
Humfanya mtu huyo, kutowawaza wengini,
Na kesho yeye ni huyo, msada ataka kwani,
Sote tukitangamana, tamaliza donda dugu.

Mengine baadhi yayo, ya ufisadi nchini,
Madonda yaumayo, pasi hata afueni,
Wakubwa wengi wayo, kula yetu maskini,
Sote tukitangamana, tamaliza donda dugu.

Jingine kanda na hayo, ubaguzi duniani,
Si wa rangi tuishiyo, au wa mali abadani,
Haya yaatua moyo, tukifia arthini,
Sote tukitangamana, tamaliza donda dugu.

WANJOHI PETER
‘Kitunguu Machoni’
Chuo Kikuu cha Mt Kenya, Thika

 

Nimegutuka, penzi silioni

Nilikuwa mshirika, nimekuweka moyoni,
Hata pesa ukitaka, ninatoa mfukoni,
Lakini nimegutuka, penzi lako silioni,
Nimekwishagutuka, kamtafute mwingine.

Kumbe wewe wanicheza, una wengi mtaani,
Pesa zangu wataka, mwenyewe hunithamini,
Sasa nimegutuka, baibai muhisani,
Nimekwishagutuka, kamtafute mwingine.

Narudi kwa mhibaka, wangu yule wa zamani,
Ambaye sina mashaka, sana ninamuamini,
Ndiye wangu mshirika, mpenzangu wa zamani,
Nimekwishagutuka, kamtafute mwingine.

Mimi nimeshakuchoka, ukweli sikutamani,
Kwako nimeshaondoka, nimerudi kwa zamani,
Yule wangu mshirika, tukae kama zamani,
Nimekwishagutuka, kamtafute mwingine.

RAMADHAN SIMBA MBOJA
Mombasa

 

Mimi ndiye kitulizo

Amepata matatizo, wangu yule wa zamani,
Na mimi habari hizo, kaniambia fulani,
Imemjaa mizozo, mingi haiwezekani,
Nimempatia maagizo, kutoka kwake fulani.

Amepatwa ni mizozo, hatujui afanye nini,
Mimi ndiye kitulizo, nimtulize rohoni,
Nyingi ya habari hizo, ni kweli sio utani,
Nimempatia maagizo, kutoka kwake Fulani.

Kutokea siku hizo, mpenzi wangu mwandani,
Ana mengi matatizo, shida hazisemeki,
Kake ndiye kimbilizo, nifanye nini jamani,
Nimempatia maagizo, kutoka kwake fulani.

Ulimwengu wa mizozo, na mwingi wa visirani,
Si ngeni habari hizo, zilianza zamani,
Twaishi na matatizo, pole binti fulani,
Nimempatia maagizo, kutoka kwake fulani.

Kamwambie mwarizo, shemejiyo wa zamani,
Awezakupa tulizo, ukaburudi rohoni,
Hayo ynagu maagizo, usipuze asilani,
Nimempatia maagizo, kutoka kwake fulani.

MWINYI JUMA AMANI JUMA
Pumwani, Nairobi