Makala

USHAURI: Ingawa wataalamu wanashauri watu kutonyoa nywele za sehemu za siri, ukiamua kunyoa fuata utaratibu huu ili kuepuka vipele

September 15th, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

NYWELE kwenye sehemu za siri huzuia maambukizi ya bakteria ambao huweza kupenya kupitia vinyweleo vya sehemu hizo.

Vilevile huzuia mchubuko wa ngozi katika sehemu hizo.

Sababu hizi hazimaanishi usinyoe nywele za sehemu za siri. Nywele zikizidi zinyoe ili kuzingatia usafi na unadhifu.

Kwa nini vipele vitokee

  • urudiaji wa wembe uliokwisha kutumia kunyoa awali au kutumia wembe wenye makali butu kama kifaa cha kunyolea
  • kunyoa uelekeo tofauti na jinsi nywele zako zinavyoota

Cha kufanya unapopata vipele

Mara nyingi vipele hivi hupotea vyenyewe baada ya muda, ila kuna vingine huwepo kwa muda mrefu na hata kuanza kuuma na kutengeneza usaha.

Unaweza kufanya mambo kadhaa.

Hakikisha unatumia kitambaa safi na maji fufutende kukanda sehemu iliyo na tatizo hilo.

Tumia asali na maji fufutende pia ili visaidie kupunguza vimelea vya bakteria wowote katika eneo hilo na hupunguza vipele hivyo.

Matumizi ya yai. Yai lina protini ziitwazo albumin ambazo husaidia sana ngozi. Kwa hiyo, husaidia kuponyesha ngozi yenye vidonda au vipele kwa haraka. Unatumia sehemu ya nje (nyeupe) ya yai kupaka sehemu husika halafu unaacha kukaukia hapo. Baada ya dakika kadhaa unabandua ambapo sehemu hiyo ya yai inatoka na kipele hasa kilichoanza kutunga usaha.

Matumizi ya sukari kama scrub. Sukari ina glycolic acid ambayo hupenya kwenye ngozi na kusaidia kuua seli zilizokufa na kuponya ngozi iliyoharibika eneo hilo haraka. Changanya sukari na mafuta ya mzeituni au ya nazi kisha paka sehemu husika na sugua taratibu kwa kuzungusha taratibu kuelekea juu kisha acha kwa muda. Halafu osha kwa maji ya ufufutende. Rudia hivi hadi vitakapokwisha.

Endapo njia hizi hazikusaidii, muone daktari wa ngozi kwa matibabu sahihi zaidi.

Unawezaje kuzuia vipele?

Tumia maji ya ufufutende uloweshe sehemu hiyo unayonyoa, kisha tumia sabuni au shaving cream kuweka povu la kutosha ili unyoe kwa urahisi zaidi kwa maana nywele zina asili ya kuota kwa kujifungafunga na ni ngumu pia, hivyo kwa kulainisha, unapunguza uwezekano wa kupata vipele.

Baada ya kulainisha, nyoa kwa kutumia wembe au mashine ya kunyolea mpya kwa uwelekeo ambao nywele zako huota.

Baada ya kunyoa ni vyema kutumia aftershave ambayo husaidia kuzuia bakteria ambao wanaweza kupenya kwenye vitundu vidogo baada ya kunyoa.

Muone daktari endapo hali hii haiishi na hasa vipele vikiendelea kutokea, vinatoa usaha, vinauma sana na vinakuwa vyekundu.