Makala

USHAURI: Jinsi ya kukabili na hata kuepuka vidonda vya tumbo

July 31st, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

VIDONDA vya tumbo vinaweza vikamsababishia madhara mtu yeyote.

Wengi wanajua  kwamba vidonda vya tumbo vinasababishwa na msongo wa mawazo (stress) na vyakula vyenye kusisimua na vyenye pilipili. Pamoja na hayo, kisababishi kikuu kingine cha vidonda vya tumbo ni bakteria ajulikanaye kama ‘Helicobacter pylori’.

Pia matumizi ya muda mrefu au ya mara kwa mara ya baadhi ya dawa za hospitali kama vile ibuprofen au aspirin nayo huchangia kutokea kwa vidonda vya tumbo.

Inachukuwa muda kufahamu ni chakula gani hasa unatakiwa kula na ni vyakula vipi hutakiwi kula.

Vyakula vikuu unavyopaswa kupenda kula ni vile vinavyoweza kufanya kupunguza asidi, gesi na sumu mwilini.

Unashauriwa kula kwa wingi matunda na mboga za majani.

Ili kupata faida hasa kwa upande huu amua na utenge mlo mmoja katika milo yako mitatu kwa siku kiasi kwamba mlo mmoja uwe ni matunda au mboga za majani pekee.

Pia pendelea kula kabeji mbichi mara kwa mara.

Ukiacha vyakula au vinywaji, tumbo lenyewe kwa asili huitengeneza asidi ili kuusaidia mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kufanya kazi yake ya kumeng’enya chakula.

Kwa ujumla kama una vidonda vya tumbo, utalazimika kuacha kabisa vitu kama pombe, sigara, sukari, soda, kahawa, chai ya rangi, vyakula vinavyosindikwa viwandani na vyakula vyenye mafuta mengi.

Kufunga kula au kuacha kula hakuwezi kukusaidia na pengine kunaweza kukuongezea vidonda zaidi.

Bila kula chochote au kukaa muda wa saa nyingi bila kula, tumbo lako linakuwa limebaki kwa sehemu kubwa na asidi tu ambayo inaweza kusababisha kuongezeka zaidi kwa vidonda vya tumbo.

Kula milo midogo midogo mingi na usikae muda mrefu bila kula na wala huhitaji kufunga kula.

Usile chakula na kulala wakati huo huo.

Usile wakati wa kulala.

Kama kweli unaumwa na vidonda vya tumbo na umeamua kupona au kuzuia usipatwe na vidonda vya tumbo huwezi kuishi hivyo.

Kama unapata maumivu ukiwa usingizini au maumivu ya vidonda vya tumbo nyakati za usiku basi wewe maliza tu kula na ujitupe kitandani, kuanzia unapokula chakula na unapoenda kulala kuwe na tofauti ya kati ya lisaa limoja hata masaa mawili.

Na ukishakula usikae chini. Ukimaliza kula tembea tembea kwa miguu hata nusu saa ndiyo utulie.

Kitendo cha kumaliza kula na ukaamua kutembea tembea huusaidia mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula kufanya kazi yake kwa kiwango chake cha juu kabisa

Unapomaliza kula na kujitupa kitandani unauzuia mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula kufanya kazi yake vizui na utaambulia maumivu zaidi ya vidonda.

Usiwaze sana kuhusu vyakula vyenye asidi. Watu wengi hujiuliza kama mwenye vidonda vya tumbo anaweza kutumia limau? Ndimu? Tangawizi? Kitunguu saumu? Machungwa? Kwa sehemu kubwa tumbo lenyewe huitengeneza asidi hata kama utakula vizuri kiasi gani.

Usiidharau msongo wa mawazo kwa sababu kuna uhusiano kati ya msongo wa mawazo na vidonda vya tumbo na kila kimoja kinaweza kumleta mwenzake.

Msongo wa mawazo unaweza kuleta vidonda vya tumbo na vidonda vya tumbo vinaweza kuleta msongo wa mawazo.

Kwa hiyo jikague na ujipeleleze ni kitu gani hasa ndicho sababu ya wewe kuwa na msongo wa mawazo na ukiondoe kwenye maisha yako bila kujali ni nini au ni nani.

Usiuguze msongo wa mawazo wala usikubali kuishi unyongeni.