Makala

USHAURI: Kuwa makini unaponunua ndizi ili kuepuka zilizoivishwa kwa kemikali

September 14th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

ILI kuwa mwenye siha bora, wataalamu wa afya wanahimiza kula chakula chenye madini kamilifu.

Madini muhimu kwenye mwili wa binadamu na ambayo hayapaswi kukosa ni Protini, Vitamini na Wanga. Mengine ni Calcium kwa minajili ya kuimarisha mifupa na Iron.

Katika orodha ya Vitamini, mbali na mboga, matunda yamesheheni madini hii. Kuna matunda tofauti kama vile machungwa, karakara, matufaha, maembe, mapapai, ndizi, zabibu, haya yakiwa machache tu kuorodhesha.

Wakulima wamekuwa wakihimizwa kukumbatia mfumo wa kilimohai.

Huu ni mfumo ambapo mimea inakuzwa bila kutumia kemikali, hasa mbolea na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa.

Magonjwa kama Saratani yanadaiwa kuchangiwa na lishe, hasa mazao yaliyozalishwa kwa pembejeo zenye kemikali. Wadau husika katika sekta ya kilimo hususan wataalamu wamekuwa wakihamasisha haja ya kufanya kilimohai ili kuepuka masaibu hayo.

Hata ingawa kuna wakulima wanaofuata ushauri huo, baadhi ya matunda yaliyokomaa na kuvunwa yanasemekana kuivishwa na kemikali.

Juliet Wanga afisa na mtaalamu wa masuala ya afya anasema mnunuzi anapaswa kuwa makini anaponunua ndizi, anazotaja zimeathirika pakubwa. “Ndizi zinapokomaa huvunwa na kusubiriwa ziive, baadhi ya wafanyabiashara wameibuka na mbinu mbadala – kutumia dawa zenye kemikali kuziivisha haraka. Hii ni hatari katika afya ya binadamu,” aonya Bi Wanga.

Ingawa ndizi zikiachiliwa kuivia shambani zinapokomaa huwa katika hatari ya kushambuliwa na wadudu, wakulima huzivuna na kuzihifadhi katika maghala. Aidha, kiwango cha joto kinachopendekezwa kufanikisha hilo ni nyuzi kati ya 14 na 16 katika kipimo cha sentigredi.

Wakulima wengi hufunika ndizi kwa majani au maganda ya migomba.

“Huyafunika kwa kuyazungushia maganda kisha ninayatia kwenye gunia na kulifunika. Huiva baada ya siku kadhaa,” asema Stephen Macheru, mkulima kutoka Nyeri.

Mtaalamu Juliet Wanga anatahadharisha kuwa baadhi ya wakulima na wafanyabiashara wanatumia njia za mkato kuivisha matunda haya.

“Kwa kawaida, ndizi zinapaswa kuiva kati ya siku tatu hadi nne. Zinapovunwa zikiwa kijani, halafu siku inayofuata zinakuwa zimeiva unafaa kuwa na wasiwasi. Kuna wanaotumia mkato kwa kuziivisha kwa kemikali,” afafanua.

Ndizi zilizoiva ni za rangi ya manjano na zingine kijani.

“Sehemu zingine za maganda husalia na michirizi ya kijani. Ndizi yote ikiwa ya manjano una haki kuitilia shaka. Dawa inapotumika kuivisha huibadilisha rangi usione ya kijani,” anaonya.

Mdau huyu anahimiza wanunuzi kuwa makini wanapochagua matunda haya sokoni. Pia, anashauri haja ya kurejelea mfumo asilia – utumizi wa majani na maganda ya migomba kuivisha ndizi.

Mbali na kuyahifadhi katika maghala, matunda haya ukiyanunua yakiwa mabichi na uyaweke sakafuni yataanza kuiva baada ya siku tatu au nne.