USHAURI NASAHA: Endeleza jitihada za kujikuza, japo kwa akali ndogo

USHAURI NASAHA: Endeleza jitihada za kujikuza, japo kwa akali ndogo

NA HENRY MOKUA

NI kawaida mwanafunzi kutamani kufanikiwa sawa na wanataaluma mbalimbali anaowaona katika ujirani wake.

Ni kawaida pia kufikiri kwamba waliofanikiwa wamefanya vile kutokana na muujiza fulani ambao yeye hajapata kuushuhudia. Hudumu kutaraji kwamba muujiza sawa na huo utatendeka kwake siku moja.

Hata hivyo ukweli ni kwamba kuyafikilia mafanikio ni tokeo la jitihada ndogondogo za kidesturi, ukipenda, za mara kwa mara.

Pana umuhimu mkubwa katika kuamua na kuanza kufuata mkondo mpya wa maisha yako; mkondo wa kuibuka na mikakati mipya uliyo na hakika itakufanikisha masomoni mwako.

Miongoni mwa mabadiliko unayostahiki kuyafanya ni kuutumia muda wako vilivyo.

Wapaswa kukoma kupiga gumzo wakati wa kulala unapowadia.

Hivi ni kwa sababu usingizi wa kutosha ni muhimu mno kwako.

Akili yako hupata fursa nzuri ya kuikuza kumbukumbu yako ya kudumu (long term memory) unapopata usingizi wa kutosha.

Kujinyima usingizi wa kutosha kwa upande wake hukuzidishia mavune (fatigue) hivi kwamba unashindwa kudumisha makini darasani.

Anza kufanya mabadiliko taratibu tokea leo – hakikisha unaanza kujizoeza kulala wakati wa kulala unapowadia.

Jambo jingine unalopaswa kulitia maanani ni kufanya mashauriano ya mara kwa mara na mwalimu wako wa somo. Nakunasihi uanze kufanya mashauriano hayo hata kwa dakika 15 kila siku.

Wanafunzi wengi hukosa kuvuna kutokana na mashauriano haya kwa kuwa huyafanya kwa siku chache kisha wakayakoma.

Ili uone matokeo ya mashauriano yako na mwalimu yafanye desturi yako.

Utaanza kuzoa alama 1 ya ziada, 5, 10 na hatimaye ndoto yako itatimia.

Aghalabu, mazingira unayojipata kwayo huwa yanakinzana na ndoto zako.

Jitahidi kuyabuni mazingira uyatakayo.

Ikiwa wenzio watahiari kupiga gumzo wakati wa kulala, wewe zoea kulala wakati ufaao. Wakiamua kutoshauriana na walimu wewe kalenge mashauriano yenyewe kwani ndiwe unajua maisha ya halafu unayoyalenga.

  • Tags

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Kauli ‘uchumi umepanda’ haina mashiko na...

Aliyetumia wilbaro kama jukwaa ni MCA

T L