Siasa

Ushawishi wa Joho kisiasa Pwani watiwa doa na kiti cha Msambweni

December 17th, 2020 1 min read

Na MOHAMED AHMED

KUSHINDWA kwa Gavana Hassan Joho wa Mombasa kuhakikisha ODM kimeshinda uchaguzi mdogo wa ubunge wa Msambweni, Kaunti ya Kwale, kumezua mjadala kuhusu iwapo ushawishi wake kisiasa umefifia.

Alipopiga kambi Msambweni, Bw Joho alisisitiza angefanya juu chini kuhakikisha mgombeji wa ODM, Omar Boga ameshinda kiti hicho.

Lakini hata baada ya kumwalika kiongozi wake Raila Odinga mara mbili kufanya kampeni eneo hilo na pia kuhakikisha Rais Uhuru Kenyatta amemwidhinisha Bw Boga, Gavana Joho alishindwa kutimiza ahadi yake kwani mgombea wa kujitegemea Feisal Bader alishinda kiti hicho.

Bw Bader aliungwa mkono na Naibu Rais William Ruto na kampeni zake zikaongozwa na Gavana Salim Mvurya wa Kwale.

Kushindwa kwa Bw Joho kushinda Msambweni kumeacha wengi wakijiuliza iwapo hiyo ni ishara ya kupoteza makali yake kisiasa hasa katika eneo kubwa la Pwani, ambako amekuwa akijipiga kifua kuwa yeye ndiye ‘Sultan’ wa ukanda huo.

Kulingana na Bw Mvurya, Bw Joho amepata funzo kuwa hawezi kulazimisha misimamo yake kwa wakazi wa Pwani.

“Hili ni funzo kwake kuwa anahitaji kuwaheshimu viongozi wengine wa Pwani,” akasema Bw Mvurya.

Mbunge wa Nyali, Mohamed Ali naye alitaja kushindwa kwa ODM eneo la Msambweni kama dhihirisho kuwa Gavana Joho amefifia kisiasa.

Lakini kiongozi wa vijana wa chama cha ODM katika Kaunti ya Mombasa, Moses Aran, alipuuzilia mbali maoni ya wapinzani wa Bw Joho akisema gavana huyo angali kigogo katika siasa za Mombasa na Pwani yote.

“Huwezi kusema Joho amefifia kwa kupoteza uchaguzi mmoja mdogo. Kama ODM tulishindwa na tumekubali, lakini hii haina maana kuwa ushawishi wake umedidimia,” akasema Bw Allan.

Akaongeza: “Baadhi ya wanaomkosoa gavana walisaidiwa naye kushinda viti wanavyoshikilia. Watu kama Aisha Jumwa wanajua Joho ndiye aliyewasaidia kuinuka kisiasa.”

Tangu matokeo ya Msambweni kutangazwa, Bw Joho hajanena lolote na wengi wanasuburi kusikia atakavyosema kuhusu kushindwa kwake kutimiza ahadi aliyompa Bw Odinga wakati kampeni za Msambweni zilipoanza.