Michezo

Ushelisheli yachezesha mpishi, madereva, waashi dhidi ya Super Eagles ya Nigeria

September 14th, 2018 2 min read

Na Geoffrey Anene

HEBU fikiria Harambee Stars inachezesha mpishi langoni, mabeki ni madereva na waashi, viungo ni maakuli na washambuliaji ni waelekezi wa watalii?

Hivyo ndivyo mambo yalikuwa timu ya Ushelisheli iliposherehekea kupigwa mabao 3-0 na Super Eagles ya Nigeria ikitumia kikosi chake thabiti kilichojumuisha watu wanaofanya kazi za kawaida wakiwemo wapishi, madereva, waashi, makuli na waelekezi wa watalii katika mechi za raundi ya pili za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 hapo Septemba 9, 2018.

Kipa wa Ushelisheli, Dave Mussard, ambaye ni mpishi katika hoteli ya Pataran katika kisiwa cha Digue, hasa ndiye alifanya kikosi hicho kipate umaarufu katika mitandao ya kijamii.

Unene wa kipa huyu mwenye umri wa miaka 31 ulimfanya afananishwe na mvamizi wa zamani wa Brazil, Ronaldo.

Tovuti ya thesouthafrican.com inasema kwamba kwa sababu timu ya Ushelisheli inashirikisha wachezaji wasiotegemea timu ya taifa kupata posho lao, wote wana kazi za pembeni. “Wachezaji waliomba ruhusa kutoka kwa waajiri wao na wakati mwingine walinyimwa ruhusa hiyo na wakakosa mazoezi,” tovuti hiyo inasema.

Imeongeza, “Beki Bertrand Esther ni dereva, naye winga Colin Bibi ni mesenja. Na Mussard, bila shaka ni mpishi. Ukiweka pamoja mapato yao ni karibu Sh64,262 kwa mwezi. Kuna marupurupu ya kufanya mazoezi, lakini madogo sana, hayatoshi kufanya iwe kazi.”

Mechi hiyo ilisimamiwa na refa Mkenya Davies Omweno. Nigeria ilibwaga wenyeji wao Ushelisheli kupitia mabao ya Ahmed Musa, Chidozie Collins na Odion Ighalo.

Kwa wiki moja, Chidozie anakula mshahara wa Sh1,063,945 katika klabu ya Nantes nchini Ufaransa, Ighalo Sh25,174,408 katika klabu ya Changchun Yatai  nchini Uchina naye Musa alikuwa Sh8,096,000 akiwa Leicester City nchini Uingereza kabla ya kuhamia Al Nasr nchini Saudi Arabia baada ya kukamilisha mkopo kutoka CSKA Moscow nchini Urusi.

Ushelisheli inavuta mkia bila alama katika Kundi E linaloongozwa na Libya na Afrika Kusini, ambazo zina alama nne kila moja. Nigeria inashikilia nafasi ya tatu kwa alama tatu.