Michezo

Ushindi kwa Butterfly, Tandaza yala sare

April 30th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

IBRAHIM Chimwani alitikisa wavu mara moja na kusaidia kikosi cha Butterfly FC kudunga Wajiji FC kwa bao 1-0 kwenye mechi ya Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili, huku Tandaza FC ikiteleza na kuachia pointi mbili muhimu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Bomas of Kenya uwanjani Lower Kabete Nairobi.

Washiriki wa kipute hicho waliendelea kuwasha moto ambapo kwa mara nyingine Karatina Homeboyz ilijikuta njia panda ilipokubali kulala kwa magoli 4-3 mbele ya Kibra United ugani Woodley Kibera, Nairobi.

”Tunashukuru wachezaji wetu kwa ushirikiano mwema dimbani pia kujiongezea pointi zote muhimu,” meneja wa Butterfly, Fredrick Ndinya alisema na kuongeza kuwa wamepania kuendeleza mtindo huo ingawa shughuli siyo rahisi.

Butterfly ambayo ni ya pili kwenye jedwali inaendelea kutoana kijasho dhidi ya Tandaza na Gor Mahia Youth. Kabla ya mchezo huo wachezaji wa Butterfly walijipiga kifua na kusema walikuwa tayari kuwafanyia mbaya wageni wao kama walivyowatendea kwenye mechi za mkumbo wa kwanza.

Kibra ilisajili ufanisi huo kupitia Billy Nyaoro aliyetikisa wavu mara tatu huku Bryon Otieno akiitingia bao moja.

Nao wafungaji wa Karatina Homeboys, walikuwa Vincent Onyango alifuma mabao mawili huku Franklin Kimathi akipiga moja safi.

Nayo Gathanga FC ilibahatika kutuzwa ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao kikosi cha Mathaithi kuingia mitini.