Michezo

Ushindi kwa Kibera United na Gogo Boys

November 18th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Kibera United na Gogo Boys kila moja ilinyamazisha wapinzani wao na kuandikisha alama tatu muhimu kwenye kampeni za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu huu.

Mchana nyavu Billy Nyaoro alipiga kombora moja safi na kubeba Kibera United kubwaga Nyahururu Griffon FC bao 1-0 kwenye mchezo uliyochezewa uwanja wa Woodley Kibera, Nairobi.

Nayo Gogo Boys ilionyesha mechi safi na kufaulu kuinyamazisha Nanyuki Youth kwa mabao 2-0 huku Butterfly FC maarufu King of Ruiru ikiteleza na kurejea makwao mikono mitupu ilipolimwa bao 1-0 na Vision FC.

Gogo iliyoshuka dimbani ikijivunia kulaza CMS Allstars mabao 2-1 wiki iliyopita iliteremsha soka safi mbele ya wafuasi wa nyumbani na kunasa ufanisi huo kupitia Ali Mohammed na Ramadhan Nassur kwa kutikisa wavu mara moja kila mmoja.

”Hatuna budi kushukuru kwa ushindi huo vijana wangu walitandaza mechi safi wakilenga kuchuna alama zote,” ofisa mkuu wa Gogo Boys, Abdul Suleiman alisema na kudokeza kuwa wamepania kujibiidisha kwa udi na uvumba kutafuta tiketi ya kupanda ngazi muhula ujao.

Naye Jimmy Wafula aliitingia South B Allstars bao la usiku na kuisadia kuzoa pointi moja baada ya kutoka sare bao 1-1 na Ruiru Hotstars.

Nayo South B Sportiff iliambulia patupu ilipodungwa mabao 2-0 na Korogocho Youth.