Michezo

Ushindi kwa Nzoia, Nakumatt, Sofapaka, Thika na Sharks KPL

May 28th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

NZOIA Sugar imeangamiza Wazito kwa mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Soka ya Kenya uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi, Mei 27, 2018.

Wanasukari hawa walikuwa katika orodha ya washindi wa mechi za raundi ya 17 iliyoshuhudia Nakumatt ikibwaga Posta Rangers 2-0, Sofapaka ikipepeta Ulinzi Stars 2-1, Vihiga United ikinyamazishwa 1-0 na Thika United na Kariobangi Sharks ikirarua Bandari 1-0 Jumapili. Tusker ililemewa 2-0 nayo Chemelil ikacharazwa 1-0 katika mechi za Mei 26.

Mchezaji anayeongoza kuchana nyavu, Elvis Rupia aliongoza Nzoia kupiga Wazito bila huruma. Rupia, ambaye ameona lango mara 12, aliweka Nzoia bao 1-0 juu dakika ya 19. Morven Otinya na Victor Omondi walihakikishia Nzoia ushindi walipojaza kimiani mabao mawili katika dakika nne za mwisho.

Kipigo hiki ni cha nne mfululizo kwa Wazito, ambayo imeingia maeneo hatari ya kutemwa. Nzoia nayo imeingia mduara wa klabu tano-bora baada ya kuzoa alama ushindi mbili, sare moja na kichapo kimoja katika mechi nne zilizopita.

Ulinzi haikubahatika kuandikisha ushindi wa tano mfululizo ilipolipuliwa 2-1 na Sofapaka katika uwanja wa Afraha kupitia mabao ya Umaru Kasumba na Kepha Aswani.

Raia wa Uganda, Kasumba aliwapa mabingwa hawa wa mwaka 2009 Sofapaka bao la ufunguzi dakika ya 33 kabla ya Aswani kuimarisha uongozi huo dakika tatu baadaye.

Elvis Nandwa alifungia Ulinzi bao la kujiliwaza dakika ya 45. Mabingwa mara nne Ulinzi walikuwa wamelemea Sofapaka mara nne mfululizo kabla ya kukosa majibu Jumapili.

Katika mechi iliyotangulia kusakatwa Jumapili, Sharks ililemea Bandari kwa mara ya tatu mfululizo, mara hii kupitia bao la Sven Yidah uwanjani Camp Toyoyo.

Kiungo huyu alifuma wavuni bao safi kupitia kichwa chake baada ya kupokea frikiki murwa kutoka kwa Duke Abuya dakika ya 55.

Sharks, ambayo ilizamisha Bandari 1-0 nyumbani na ugenini mwaka 2017, haikulegeza ulinzi wake hadi kipenga cha mwisho.

Vijana wa kocha William Muluya hawajapoteza mechi sita. Bandari imeambulia alama mbili pekee katika mechi zake nne za mwisho.

Nakumatt iliendelea na shughuli ya kujinasua kutoka mduara hatari wa kutemwa ilipoadhibu Rangers 2-0 kupitia mabao ya Boniface Mukhekhe uwanjani Camp Toyoyo.

Mukhekhe alitikisa nyavu dakika ya tisa na 78. Ni ushindi wa pili mfululizo wa Nakumatt wa 2-0 dhidi ya Rangers ambayo matokeo yake mazuri dhidi ya Nakumatt ni sare tasa Mei 14 mwaka 2017.

Nakumatt ina ushindi tatu na sare moja katika mechi zake nne zilizopita. Rangers haina ushindi katika mechi tano baada ya kuambulia sare tatu na vichapo viwili.

Shami Kibwana alisaidia Thika kukanyaga wenyeji Vihiga United 1-0 mjini Mumias. Alicheka na nyavu dakika ya nane. Vihiga ilikuwa imezima Wazito 2-1 na SoNy Sugar 2-0 kabla ya kupigwa breki na Thika, ambayo iliingia mchuano huu ikiuguza kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa AFC Leopards.