Michezo

Ushindi wa 1-0 waipa Bayern kombe la 8 mfululizo

June 17th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BAYERN Munich walisheherekea ushindi wao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa msimu wa nane mfululizo ndani ya uwanja mtupu wa Weser baada ya kuwachabanga Werder Bremen 1-0 mnamo Juni 16, 2020.

Nyota Robert Lewandowski alifungia Bayern bao hilo la pekee kunako dakika ya 43 baada ya kushirikiana vilivyo na beki Jerome Boateng.

Chini ya kocha Hansi Flick, Bayern walinyakua ufalme wa Bundesliga msimu huu wakisalia na mechi mbili zaidi za kusakata.

Mechi dhidi ya Werder ilikuwa yao ya 11 mfululizo kusajili katika kampeni za Bundesliga muhula huu, na ushindi huo uliwadumisha kileleni kwa alama 10 zaidi kuliko Borussia Dortmund ambao wana mechi tatu zaidi za kutandaza kabla ya msimu huu kutamatika rasmi.

Bayern walikamilisha mechi dhidi ya Werder wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya beki Alphonso Davies kufurushwa uwanjani kwa kadi nyekundu kwa kosa la pili lililompa kadi ya manjano.

Lewandowski ambaye ni nahodha wa Poland, kwa sasa anajivunia jumla ya mabao 31 katika Bundesliga msimu huu, rekodi ambayo inafikia ile iliyowekwa na Pierre-Emerick Aubameyang akiwatandazia Dortmund katika kivumbi cha Bundesliga mnamo 2016-17 kabla ya kuyoyomea Arsenal. Idadi hiyo ya mabao ndiyo ya juu zaidi kuwahi kufungwa na mchezaji wa kigeni katika soka ya Bundesliga.

Bayern walipotawazwa mabingwa wa Bundesliga msimu jana, walifanya hivyo katika siku ya mwisho ya kampeni baada ya kusajili ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt mbele ya mashabiki 75,000 ugani Allianz Arena.

Mnamo Juni 16, 2020 walipotwaa ubingwa wa muhula huu, hapakuwapo na mashabiki katika uwanja wa Weser ulio na uwezo wa kubeba hadi mashabiki 42,000 walioketi.

Bayern ambao wanawania jumla ya mataji matatu msimu huu, wamesalia na mechi mbili za Bundesliga dhidi ya Freiburg nyumbani na Wolfsburg ugenini.

Kwa sasa wanafukuzia pia taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na wamo katika nusu-fainali za German Cup ambapo watakutana na Bayer Leverkusen mwishoni mwa Juni 2020.

Baada ya kudhalilishwa kwa kichapo cha 5-1 kutoka kwa Eintracht Frankfurt mnamo Novemba 2, 2019, Bayern walijipata katika nafasi ya nne jedwalini kwa alama nne zaidi nyuma ya viongozi wa wakati huo, Borussia Monchengladbach.

Matokeo hao duni yaliwachochea Bayern kutamatisha uhusiano wao wa miezi 16 na kocha Niko Kovac na nafasi yake kutwaliwa na Flick aliyetia saini mkataba mpya wa miaka mitatu mnamo Aprili 2023.